Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Wallace Karia ameunda Kamati ya Tuzo za Ligi Kuu ya Vodacom  Tanzania Bara msimu wa 2017/18.

Kamati hiyo itaongozwa na Mwenyekiti Ahmed Mgoyi wakati Makamu Mwenyekiti ni Almas Kasongo ilihali  Amiri Mhando ameteuliwa kuwa Katibu wa kamati hiyo ya tuzo.

 

Mhando ni Mhariri wa Gazeti la Spotileo linalotolewa na Kampuni ya Magazeti ya Serikali - Tanzania Standard Newspaper (TSN).

 

Wajumbe ambao wameteuliwa ni Ibrahim Kaude; Mkuu wa Kitengo cha Michezo katika Kampuni ya Azam Media, Patrick Kahemele na Kocha mkongwe wa soka, Kenny ‘Mzazi’ Mwaisabula.

 

Kadhaika Mhariri Mtendaji wa Kampuni ya Uchapishaji ya Global (Global Publisher inayochapisha magazeti kadhaa likiwamo Championi), Saleh Ally; Mtangazaji mahiri wa michezo kutoka Kituo cha Redio cha EFM, Ibrahim Masoud na Mtangazaji wa Vipindi katika Kituo cha Radio ya Watu, Fatma Likwata.

 

Pia wamo Mwandishi Mwandamizi wa Michezo wa Gazeti la Mwanaspoti linalochapishwa na Kampuni ya Mwananchi Communication (MCL), Gift Macha; Katibu Mkuu wa Chama cha Wachezaji wa Mpira wa Miguu, Said George na Mhariri wa Michezo wa Gazeti la HabariLeo linalotolewa na TSN, Zena Chande.