Mechi mbili za Ligi Kuu ya Vodacom zinatarajiwa kufanyika Desemba 31, 2016 na mbili za zitafungua mwaka 2017 ambako Kituo cha Televisheni cha Azam - Wadhamini wenza wa ligi hiyo, wamethibitishia Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) kupata burudani kwa michezo yote kulingana na ratiba.

Katika Ligi hiyo ambayo pia inadhaminiwa na Benki ya Diamond Trust (DTB) kama Mdhamini Mwenza, michezo yote inatarajiwa kuanza saa 10.00 jioni na Burudani kwa Wote kupitia Azam Tv ya King’amuzi cha Azam itaonyesha michezo miwili Desemba 31, mwaka huu kadhalika ile miwili ya Januari mosi, 2017.

Kesho Desemba 31, mwaka huu Mwadui ya Shinyanga itacheza na Kagera Sugar ya Kagera kwenye Uwanja wa Mwadui mkoani Shinyanga katika mchezo Na.  141.

Kamishna anatarajiwa kuwa Nassib Mabrouk wa Mwanza na Mwamuzi ni Isihaka Mwalile na wasaidizi wake ni Hellen Mduma na Omary Kambangwa – wote kutoka Dar es Salaam. Julius Kasitu wa Shinyanga anatarajiwa kuwa Mwamuzi wa Akiba.

Kadhalika siku ya kufunga mwaka 2016, Timu ya Mbeya City inatarajiwa kucheza na Mbao FC kwenye Uwanja wa Sokoine jijini Mbeya katika Mchezo Na. 143 ambao msimamizi wa mchezo atakuwa Joseph Mapunda wa Ruvuma.

Mwamuzi katika mechi hiyo anatarajiwa kuwa Hussein Athuman wa Katavi wakati wasaidizi wake watakuwa ni Lulu Mushi wa Dar es Salaam na Nicholaus Makaranga wa Morogoro. Mwamuzi wa Akiba Mezani atakuwa Mashaka Mwandembwa wa Mbeya.

Januari mosi kutakuwa na michezo miwili tu ya kukaribisha Mwaka Mpya ambako Toto African ya Mwanza itacheza na Stand United ya Shinyanga kwenye Uwanja wa CCM Kirumba katika mchezo Na. 144 utakaosimamiwa na Jovin Bagenda wa Kagera. Mwamuzi atakuwa Israel Nkongo sambamba na wasaidizi wake Soud Lila na Frank Komba, wote wa Dar es Salaam. Mwamuzi wa akiba mezani atakuwa Mathew Akrama wa Mwanza.

Pia African Lyon ya Dar es Salaam itakuwa mwenyeji wa JKT Ruvu katika mchezo Na. 142 utakaofanyika Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam. Kamishna atakuwa Hamisi Kitila wa Singida wakati Mwamuzi anatarajiwa kuwa Selemani Kinugani wa Morogoro wakati wasaidizi wake ni Omary Juma wa Dodoma na Agnes Pantaleo wa Arusha wakati mezani atakuwa Shafii Mohammed wa Dar es Salaam.

Mara baada ya michezo hiyo, Ligi Kuu ya Vodacom itasimama kwa wiki mbili kupisha michuano ya Kombe la Mapinduzi inayotarajiwa kuanza Januari mosi, mwaka huu.

..…………….…………………………………………………………………..............

IMETOLEWA NA SHIRIKISHO LA MPIRA WA MIGUU TANZANIA (TFF)