Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF), limeteua waamuzi wanne wa Tanzania watakaokwenda kuchezesha mechi ya Ligi ya Mabingwa Afrika kati ya timu za A Porto Louis 2000 ya Mauritius na El Hilal ya Sudan wikiendi ijayo.

 

Katika mchezo huo ambao utafanyika ama Machi 17, 18 au 19 Mwamuzi wa kati atakuwa Israel Mujuni Nkongo wakati wasaidizi wake watakuwa ni Samuel Hudson Mpenzu na Josephat Deu Bulali huku Mwamuzi wa akiba akiwa ni Elly Ally Sasii.


Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL), inatarajiwa kuendelea keshokutwa Jumatano ambako mabingwa watetezi wa taji hilo, Young Africans itaalikwa na Ruvu Shooting kwenye mchezo utakaofanyika Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

 

Mbali ya mchezo huo mmoja kwa siku ya Jumatano, ligi hiyo ambayo ni michuano mikubwa nchini, itaendelea mwishoni mwa wiki hii ambako kwa siku ya Jumamosi Machi 4, mwaka huu Simba itacheza na Mbeya City kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.


Timu nne vinara wa Ligi Daraja la Pili kutoka makundi manne, zinatarajiwa kuanza kupambana keshokutwa Jumatano - Machi mosi, mwaka huu ‘Play off’ kutafuta timu Tatu Bora, zitakazopanda daraja kucheza Ligi Daraja la Kwanza msimu wa 2017/2018.

Timu hizo zilizofanya vema ni pamoja na JKT Oljoro ya Arusha, Cosmopolitan ya Dar es Salaam, Mawenzi ya Morogoro na Transit Camp ya Shinyanga. Ziliibuka vinara katika makundi yao.


Ligi Kuu ya Mpira wa Wanawake, hatua ya timu sita Bora (6), ilianza rasmi jana kwa Mlandizi Queens ya Pwani kuilaza JKT Queens ya Dar es Salaam mabao 3-2 katika mchezo wa awali mchana kabla ya ule wa jioni Sisterz ya Kigoma kuifunga Fair Play ya Tanga mabao 5-1.

 

Ligi hiyo inayochezwa Kituo kimoja cha Uwanja wa Karume, Ilala Dar es Salaam inakutanisha timu sita zinazowania ubingwa wa ligi hiyo ya wanawake ambayo inafanyika kwa mara ya kwanza nchini Tanzania. Pia ni ya kwanza kwa nchi za Afrika Mashariki.


Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Jamal Emil Malinzi ameelezea mikakati mbalimbali ya maendeleo ya soka nchini akisema hiyo ndiyo sababu ya Kamati ya Utendaji kubuni na kuunda Mfuko wa Maendeleo ya soka.

 

Katika Risala yake aliyoitoa jana mbele ya Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mheshimiwa Nape Nnauye katika uzinduzi wa mfuko huo, Rais Malinzi alisema wamefanya hivyo kwa lengo la kutimiza ndoto za Tanzania kushiriki michuano mbalimbali ya soka.