Makocha wa timu ya Taifa ya Mpira wa Miguu ya vijana wa Tanzania ‘Serengeti Boys’, Bakari Nyundo Shime na Muharami Mohammed anayewanoa makipa watatu wa timu hii, wamesema kwa pamoja: “Tuko tayari kwa vita.”

Shime maarufu kama Mchawi Mweusi, amezungumza hayo wakati anaendelea kufanya maandalizi ya mwisho ya mchezo dhidi ya Jamhuri ya Congo utakaofanyika Jumapili Oktoba 2, kwenye Uwanja wa Alphonse Massamba-Débat ulioko kwenye Makutano ya Barabara za Nkolo na Boko, hapa jijini Brazzaville.

Kamati ya Katiba, Sheria na Hadhi za wachezaji imetoa siku tatu kuanzia jana Septemba 24, 2016 kwa viongozi wa klabu za Simba SC na Young Africans SC kukaa chini na kumaliza suala la usajili wa mchezaji Hassan Ramadhani Kessy kwa njia ya mazungumzo ya kuelewana.

Hatua hiyo imefikiwa baada ya mjadala wa muda mrefu kuhusu kesi mbili zilizofunguliwa na Simba mbele ya kamati hiyo inayoongozwa na Mwanasheria Richard Sinamtwa. Kesi ya kwanza iliyofunguliwa na Simba SC ni dhidi ya Young Africans kudaiwa kuingia mkataba na mchezaji Hassan Kessy wakati bado ana mkataba na Simba SC.

Timu ya Mpira wa Miguu ya Tanzania (Taifa Stars), inatarajiwa kucheza na Ethiopia katika mchezo wa kirafiki wa kimataifa Oktoba 8, 2016.

Mchezo huo utakaofanyika jijini Addis Ababa, umeratibiwa kwa mujibu wa kalenda ya Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA) ambalo huwa na kalenda ya wiki ya mechi za kimataifa kwa wanachama wake – Tanzania ni miongoni mwao. Shirikisho la Mpira wa Miguu la Ethiopia (EFF), wameomba mchezo huo ufanyike kwao.

Ubingwa Kombe la CECAFA Chalenji kwa timu za mpira wa miguu za wanawake katika nchi za Afrika Mashariki, umewavutia wadau wengi kwa kiwango kikubwa hivyo kushusha neema kwa wachezaji hao wa timu ya taifa ya Tanzania Bara maarufu kama Kilimanjaro Queens ambayo imeandika historia ya kutwaa taji hilo ikiwa ni taifa la kwanza katika mashindano hayo mapya.

Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Nape Nnauye, amefurahishwa na ubingwa wa timu hiyo akisema: “Si ubingwa tu, bali umefuta dhana ya Wakenya ambao siku zote wamekuwa wakitangaza Mlima Kilimanjaro uko kwao Kenya wakati upo hapa Tanzania. Kwa kuifunga Kenya, mmefanya kazi nzuri.”

Ligi Daraja la Kwanza (FDL) inaanza wikiendi hii ambako katika kundi A, mchezo wa kwanza unapigwa leo Ijumaa Septemba 23, 2016 kwa kuzikutanisha timu za Ashanti United ya Ilala, Dar es Salaam na Pamba ya Mwanza katika mchezo utakaopigwa Uwanja wa Karume jijini.

Kwa mujibu wa ratiba, michezo mingine itachezwa kesho Septemba 24, 2016 kwa kuzikutanisha timu za Lipuli dhidi African Sports utakaofanyika Uwanja wa Kichangani mjini Iringa. Mchezo huo utakuwa ni wa kundi A wakati katika kundi B michezo itakuwa ni kati ya Kurugenzi ya Iringa dhidi ya KMC ya Kinondoni kwenye Uwanja wa Wambi ulioko Mafinga. Mlale JKT itaikaribisha Njombe Mji kwenye Uwanja wa Majimaji mjini Songea.