Msuluhishi wa kisheria wa sakata la madai ya Simba dhidi ya Young Africans hali kadhalika Mchezaji Hassan Hamisi Ramadhani maarufu kama Hassan Kessy, Wakili Msomi, Mzee Said El-Maamry anatarajiwa kukutana na pande zinazopingana Alhamisi Novemba 3, mwaka huu ili kufikia mwafaka wa mwadai hayo.

Kamati ya Katiba, Sheria na Hadhi za Wachezaji iliagiza pande za Simba na Young Africans kumaliza suala hilo mapema mwezi uliopita, lakini kwa sababu zilizo nje ya TFF na Kamati yake walishindwa kufanya hivyo kupewa barua ya wito kuitwa kikaoni Oktoba 29, mwaka huu.

Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL) inatarajiwa kuendelea kesho kwa viwanja sita ambako kwa mara ya kwanza timu zote za Dar es Salaam zitakuwa mikoani kupambana kutafuta nafasi bora katika ligi hiyo iliyoanza Agosti 20, 2016 kabla kufifikia ukomo wa mzunguko wa 15, Novemba 12, mwaka huu.

Vinara ligi hiyo kwenye msimamo msimu wa 2016/17, Simba SC watakuwa wageni wa Stand United kwenye Uwanja wa CCM Kambarage wakati mabingwa watetezi wa taji hilo Young Africans itakaribishwa na Mbeya City kwenye Uwanja wa Sokoine jijini Mbeya.

Baada ya kukosa mchezo wa kirafiki wa kimataifa dhidi ya Ethiopia, timu ya Taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’ imepata mwaliko wa kucheza na Zimbabwe katika mchezo wa kirafiki wa kimataifa unaotarajiwa kufanyika jijini Harare, Novemba 13, mwaka huu.

Kama ilivyotokea kwa Ethiopia kuomba nafasi hiyo kwa Tanzania, pia Zimbabwe imefanya hivyo na mara moja Tanzania imethibitisha kucheza mchezo huo wa kirafiki wa kimataifa wenye kutoa tathmini ubora ili kuingia kwenye viwango vya ubora vya Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA).

Timu ya Taifa ya Mpira wa Miguu ya vijana wenye umri wa chini ya miaka 17 – Serengeti Boys, imeanza rasmi kambi ya wiki moja kabla ya kwenda Korea Kusini ambako itashiriki michuano maalumu ya kimataifa iliyoandaliwa na Shirikisho la Mpira wa Miguu la Korea Kusini.

Timu hiyo itapiga kambi kwa wiki moja kwenye Hosteli za TFF zilizoko Uwanja wa Kumbukumbiu ya Karume, Ilala jijini Dar es Salaam. Tayari vijana wameripoti kwenye hosteli hizo tangu jana Oktoba 31, 2016.

Wadau mbalimbali wakiwamo Wajumbe wa Kamati ya Utendaji wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania, wamemwagia sifa na pongezi Rais wa TFF Jamal Malinzi kwa kuteuliwa kwake kuunda jopo la watu 11 tu wa Kamati maalumu ya mageuzi ya muundo wa CAF itakayokuwa na jukumu la kufanya mabadiliko mapya ya shirikisho.

Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF), Issa Hayatou ameteua Rais Malinzi ikiwa ni sehemu ya maazimio ya mkutano uliopita wa kawaida wa shirikisho uliofanyika Septemba 29, mwaka huu ambako Rais Hayatou amezingatia mjadala uliolenga kufanya mabadiliko kwa kufanyia kazi mara moja.