Ndugu wapenzi na wadau wa mpira wa miguu Tanzania.

Nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu muweza wa yote. 

Ni jambo la heshima na fahari kwa Shirikisho letu la mpira wa miguu Tanzania TFF kuweza kuwa na tovuti ya kisasa kama hii. 

Ndugu msomaji ninakushukuru kwa kuitembelea. Ndugu zangu, hii tovuti ni yetu sisi sote, tuitumie kwa kupashana habari, kuelemishana na pia kuburudishana kwa mikanda mbali mbali mifupi ya matukio ya michezo itakayoukuwa inawekwa hapa.

Tovuti hii itakuwa ni chombo chenu cha kuwapeni wasomaji fursa ya kujua nini kinaendelea TFF, na pia kuwapeni fursa ya kuchangia maendeleo ya mpira wetu kwa kutoa ushauri na maoni mbali mbali.

Changamoto ni jambo la kawaida Viongozi kukutana navyo, hivyo wadau wa mpira msisite kutukosoa pale mnapoona hatuendi vizuri. Kikubwa ni staha, tukosoane, tuelimishane lakini kwa staha.

Ninapenda nigusie mambo machache yaliyoko mbele yetu yanayohusiana na maendeleo ya mpira wetu.

Kama mnavyofahamu kote duniani, chimbuko la maendeleo ya mpira wa miguu iwe ni ngazi ya vilabu au ngazi ya timu za Taifa ni uwekezaji katika mpira wa watoto na vijana.

Tanzania tumepata nafasi ya kuwa wenyeji wa michuano ya Vijana Afrika chini ya miaka 17, mwaka 2019.

Natumia fursa hii kulishukuru Shirikisho la Soka barani Afrika - CAF kwa kutupa nafasi hiyo uenyeji, na sisi kama TFF tumeshaanza maandalizi ya kuelekea kwenye fainali hizo za vijana.

Jumapili Juni 7, 2015  TFF itazindua michuano ya vijana jijini Mwanza wenye umri chini ya miaka 13 itakayoshirikisha mikoa yote ya Tanzania, lengo ikiwa ni kuchagua/kunga’amua vipaji vitakavyounda timu ya Taifa U17 mwaka 2019.

Kwa kushirkiana na serikali, wadau na familia ya mpira wa miguu nchini ninaamini tutafanikiwa katika kuandaa michuano hiyo mikubwa Afrika ya vijana wenye umri chini ya miaka 17.

Nitumie fursa hii kuyaomba makampuni, taasisi, na mashirika mbalimbali kujitokeza kudhamini/kufadhili programu hiyo ya vijana chini ya miaka 13 kuelekea kwenye fainali za U17 mwaka 2019.