Bodi ya ligi yasimamisha ligi zote Tanzania Bara

Afisa Mtendaji Mkuu wa Bodi ya ligi Tanzania Bara, ndugu Almasi J. Kasongo kwa niaba ya makubaliano ya pamoja ya kikao cha bodi hiyo, amesema kuwa michezo na mashindano yote
yanayosimamiwa na bodi hiyo ya ligi Tanzania yamesimamishwa mpaka hapo serikali itakavyo toa tamko kuhusu hali ya afya nchini kuwa ni salama salimini.

Maamuzi hayo ya kikao cha Bodi yamekuja kufuatia mlipuko wa Virus vya ugonjwa wa Corona uliongia Tanzania tangu serikali ilipotangaza kuwepo kwa mgonjwa mmoja tarehe 16, Machi 2020 ambapo kufikia tarehe 18 Machi idadi ya wangonjwa iliogezeka na kufikia 3.

Akitoa ufafanuzi zaidi kuhusu suala la usimamishwaji wa ligi nchini, Kasongo amesema ligi hiyo itasimama kwa muda wa siku thelathini kama serikali ilivyo agiza, huku akiitaja sababu kuu ikiwa ni ili kupunguza uwezekano wa kuzidi kuenea kwa virus hivyo hatari vya Corona ambavyo husambaa kwa kasi tena kwa njia ya hewa, hasa sehemu zenye mkusanyiko wa watu wengi.

Amesisitiza kuwa kufungwa kwa ligi kutaondoa ama kupunguza mikusanyiko hiyo na hivyo kuweza kuokoa maisha ya wapenzi wa mipira na watanzania wengi.

Aidha Afisa Kasongo amebayanisha ya kuwa hata mara tu baada ya siku hizo thelathini kukamilika na serikali kutangaza watu kurejea kwenye shughuli zao za michezo kama kawaida bado bodi imekubaliana kuwa kutakuwa na utaratibu maalum wa wachezaji wote kufanyiwa vipimo kabla ya kurejea kujiunga na kambi katika vilabu vyao.

Kufanya hivyo kutasaidia kubaini hali ya afya za wachezaji na kuepuka kuambukizana endapo kutakuwa na wale wenye maambukizi ya virus hivyo vilivyo tishio ulimwenguni kote.