Kozi ya uongozi na utawala wa Mpira wa Miguu kwa wanawake yahitimishwa Jijini Dar es Salaam.

Kozi ya utawala na uongozi katika masuala ya Soka la wanawake iliyoanza tarehe 15 Septemba katika ukumbi wa mikutano wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania uliopo Karume Jijini Dar es Salaam imefungwa rasmi tarehe 19 Septemba, 2020 na Ofisa Masoko na Uhusiano wa Benki ya KCB (Kenya Commercial Bank) Bi. Christina Manyenye.

Bi Christina alisema kuwa anaishukuru TFF kwa kuwapa heshima ya kufunga kozi hiyo muhimu ambayo anaamini italeta mabadiliko makubwa katika tasnia ya michezo hasa katika soka la wanawake.

Hata hivyo, aliwaasa washiriki wote kuwa na tabia ya uthubutu na kujiamini kuwa wanaweza na kutokusubiri kuwezeshwa kila wakati, bali muda mwingine wainuke na kuzifuata fursa zilipo hata kama patakua na ugumu kiasi gani wakijiamini wanaweza kufanya mambo makubwa na hiyo ndio sifa ya kiongozi bora na makini.

Naye Mkufunzi wa kozi Daktari Henry Tandau akihitimisha kozi hiyo aliwapongeza washiriki wote kwa Kijitoa na kuhudhuria kozi hiyo tangu mwanzo hadi mwisho na kuwasisitiza kuwa vyeti walivyotunukiwa visiishie kukaa ukutani kama pambo bali elimu waliyoipata wakaitumie ipasavyo ili iweze kuleta matokeo chanya katika mchezo wa mpira wa miguu nchini.

Nao baadhi ya washiriki wa kozi hii waliushukuru uongozi wa TFF unaongozwa na Rais Wallace Karia na katibu Mkuu Kidao Wilfred kwa kuanzisha na kuratibu kozi hii, kwani imekuja kwa wakati muafaka na kwamba itakua msaada mkubwa kwao katika kuendesha shughuli zao mbalimbali pindi watakaporejea katika majukumu yao ya kikazi na majumbani pia. Hii ni kwa sababu suala la uongozi haliishii makazini tu bali hata katika jamii inayowazunguka wanapaswa kuishi kama mfano.

Na wengine wakajazia kwamba wamefurahishwa sana na somo la masoko na namna ya kutafuta wadhamini kwani ndio eneo ambalo limekua likiwasumbua hasa unapofika wakati wa kutangaza klabu zao na bidhaa zake na mara nyingi wanashidwa kupata udhamini; hivyo, kozi hiyo imewafungua ufahamu na sasa wamejua mbinu zote za kufanya na kwamba kilichobaki ni utekelezaji tu wa walichokisoma darasani.

Baadhi ya masomo yaliyofundishwa katika kozi hiyo yalikua ni historia ya chama cha mpira wa miguu duniani FIFA, elimu ya fedha, mambo ya utawala elimu ya masoko na namna ya kutafuta wadhamini, elimu kuhusu rasilimali watu na mchango wao katika taasisi.

Masuala mengine yaliyofundishwa ni pamoja na elimu ya kuratibu mashindano na jinsi ya kutafuta mashabiki wapya lakini pia namna ya kuwashika ili waendele kuwa waaminifu katika bidhaa au huduma ambayo taasisi inaitoa.

Kozi hiyo ya utawala na uongozi itahusisha mikoa kumi inayojumisha mikoa ya Tanzania Bara na Visiwani, hivyo basi tamati ya kozi hii katika mkoa wa Dar es Salaam ndio mwanzo wa kozi hiyo katika mkoa unaofuata ambao ni mkoa wa Tanga.