Simba Queens, Yanga Princess hakuna mbabe

Ligi kuu ya wanawake imeendelea  leo Machi 22, 2023 Kwa mechi kadhaa kupigwa katika viwanja mbambali  huku wababe Simba Queens wakiondoka na alama moja katika dimba la Uhuru baada ya kutoka sare ya goli 1-1 na timu ya Yanga Princess.

Mchezo huo ulianza kwa timu zote mbili kucheza kwa kasi ya kawaida lakini baadae Simba Queens ilionekana kuutawala mchezo na kupelekea goli kupatikana katika Dk.ya 29 kupitia kwa mchezaji Jentrix Shikangwa. Matokeo yaliendelea kusalia hivyo hadi kipindi cha Kwanza kinamalizika.

Kipindi cha pili kilianza, na Yanga Princess walionekana kuimarika wakipeleka mashambulizi katika lango la Simba Queens na kupelekea timu hiyo  kupata goli la kusawazisha  katika Dk ya  80 .Goli  hilo lilifungwa na mchezaji Wogu Chioma na kufanya  mtanange huo kumalizika Kwa sare ya goli 1-1. Matokeo ya Leo yanajirudia Kwa mara nyingine tena baada ya timu hizo mbili kutoka sare  ya goli  1-1 katika mchezo wa mzunguko wa Kwanza uliopigwa katika uwanja wa Benjamin Mkapa mwezi Disemba.

Kocha mkuu wa Simba Queens Charles Lukula alisema ” Tunamshukuru Mungu Kwa kupata alama moja, tunakwenda kusahihisha mapungufu ya leo na kujipanga Kwa mechi ijayo. Nikiri Yanga princess walikua bora kipindi cha pili na tulifanya makosa yaliyowapa faida lakini  bado nina imani na kikosi changu na mbio za ubingwa zinaendelea”.

Naye Kocha msaidizi wa Yanga Princess Fredy Mbuna aliwapongeza wachezaji wake kwa mchezo wa Leo  ambao wamefanikiwa kuondoka na alama 1 huku akisema dabi imeisha sasa wanakwenda kujipanga Kwa michezo inayofuata.

Kwa matokeo hayo ya sare ya 1-1 aliyoipata Simba Queens dhidi ya Yanga Princess yanamshusha hadi nafasi ya tatu katika msimamo wa ligi akifikisha alama 27  wakati Yanga Princess yeye akiendendelea kusalia katika nafasi Ile Ile ya nne kwa alama 22. Fountain Gate Princess anapanda juu kileleni baada ya kupata ushindi wa goli 2-1 dhidi ya Mkwawa Queens akifikisha alama 29 na JKT Queens nayo inasogea nafasi ya pili baada ya kuifunga Baobab Queens magoli 3-0 na kufikisha alama 28.