TFF NBC Mitano Tena

Shirikisho la mpira wa miguu Tanzania TFF limesaini mkataba mwingine wa Bilioni 32.56 kwa miaka mitano na benki ya NBC Agosti 11, 2023.

Mkataba huo ulioambatana na hafla fupi umefanyika kwenye ukumbi uliopo hoteli ya Tanga Beach jijini Tanga ambapo Rais wa TFF Wallece Karia, Mkurugenzi Mtendaji wa NBC Theobald Sabi, viongozi wengine kutoka TFF na Bodi ya ligi Tanzania pamoja na wawakilishi wa vilabu vya ligi kuu wote walikuwa sehemu ya wahudhuliaji.

Awali mwaka 2021 TFF iliingia mkataba wa takribani Bilioni 9 na benki hiyo na kuwapatia haki ya kuwa wadhamini wakuu liki kuu ya NBC ambayo imeongezeka ubora zaidi hata kufikia nafasi ya tano kwenye ligi za Afrika.

Akizungumza wakati wa hafla hiyo Rais Karia alisema kuwa kwa TFF udhamini huo ni zaidi ya ongezeko la thamani ya kifedha bali ni uthibitisho wa imani kubwa kwa uwekezaji wa maono waliyo nayo kwenye kukuza, kuendeleza na kusimamia mpira wa miguu nchini.

“Kulikuwa na kilio cha muda mrefu kwa ligi zetu nyingine mbili ambazo ni za kitaifa Championship na First Division League, kwa hiyo kwenye makubaliano haya yatakwenda mpaka kwenye mashindano hayo” alisema Rais Karia.

Aliongeza kusema kuwa anaamini uwekezaji huo utakwenda kuongeza ubora kwenye ligi ya Championship na kufanya ligi hiyo kuwa yenye ufanisi wa hali ya juu na hata kuwa sehemu bora ya utunzaji na kutangaza vipaji vya vijana wengi nchini.

Kwa upande wa Mkurugenzi Mtendaji wa NBC Theobald Sabi naye alisema kuwa amefurahi na kujivunia kuingia makubaliano kwa mara nyingine na TFF kwani kipindi chote wakiwa ni wadhamini wakuu wa ligi kuu Tanzania Bara kwa upande wao wamenufaika kwa kiwango cha juu kibiashara.

Sambamba na hayo Bwana Theobald anajivunia kuwa sehemu ya ongezeko la ajira katika maeneo tofauti hasa kwenye mpira kwani wanaamini kuna Wachezaji, Madaktari wa timu, Makocha, Viongozi wa timu na maeneo wameajiriwa kutokana na uwekezaji wa benki yao.

Maeneo ambayo mkataba huo umekusudia ni; makubaliano ya kuongeza miaka mitano zaidi, Uwekezaji wa Bilioni 32.56, Udhamini wa ligi daraja la kwanza ambayo bado haijapatiwa jana maalum tangu kuingia kwa makubaliano hayo pamoja na udhamini wa ligi ya vijana (U20) ambayo itaitwa NBC Youth League.