MABINGWA watetezi wa kombe la Ligi ya Wanawake, JKT Queens jana katika Uwanja wa Nyamagana waliifunga timu ya Marsh mabao 8-0 kwenye mchezo wa ligi maarufu kama Serengeti Lite Women’s Premier League.

Wakati wao wakifanya hivyo mahasimu wao Simba Queens wao walipoteza mchezo wao jana mbele ya Panama kwa kufungwa mabao 2-1 Uwanja wa Karume, Sisterz FC walishinda 3-1 dhidi ya Tanzanite SC, Mlandizi Queens alishinda kwa mabao 5-1 dhidi ya EverGreen Queens.

Kwa matokeo hayo JKT Queens anazidi kujikita nafasi ya kwanza akiwa na pointi 27, Sister FC nafasi ya pili pointi 20, Mlandizi Queens nafasi ya tatu Pointi 19, Alliance Girls nafasi ya nne pointi 17 huku Simba Queens wakiwa nafasi ya tano wakifuatiwa na Panama FC nafasi ya sita wote wana pointi 16.

Yanga Princess anashika nafasi ya 7 akiwa na pointi 12, nafasi ya nane ni Tanzanite FC na tisa ni Baobab Queens wakiwa na pointi tisa huku Marsh Academy ikiwa nafasi ya 10 na pointi sita wakati nafasi ya 11 ikichukuliwa na EverGreen Queens na ile ya 12 ikishikwa na Mapinduzi Queens wote wana pointi mbili.