Dar es Salaam.Mashindano ya Soka la ufukweni yanatarajia kuanza kutimua vumbi kesho nchini, kwa kuzikutanisha timu za Tanzania, Uganda, Malawi na Seychelles mashindano hayo yatafanyika uwanja wa Coco Beach na hakuna kiingilio chochote.

Kocha wa timu ya Taifa ya ufukweni, Boniface Pawasa alisema mashindano hayo yana maana kubwa kwao katika maandalizi ya mashindano ya Mataifa ya Afrika yatakayofanyika Desemba 8 nchini Misri.

“Haya ni maandalizi yetu kwaajili ya Afcon ya ufukweni ambayo itaanza mwezi ujao, kwahiyo kitakuwa ni kipimo kizuri ambacho kitatusogeza na kujua mapungufu yetu,” alisema beki wa zamani wa Simba, Pasawa.

Katika fainali za Mataifa Afrika, Tanzania imepangwa Kundi B pamoja na mabingwa watetezi Senegal, Nigeria, Libya. Kundi A linaundwa na wenyeji Misri, mabingwa wa zamani Madagascar, pamoja na Morocco na Ivory Coast.

Katika mashindano ya Afrika, Tanzania itakata utepe kwa kucheza dhidi ya Libya Desemba 8, kabla ya kuwavaa mabingwa watetezi Senegal Desemba 9, na kumaliza na Nigeria Desemba 10.

Fainali hizo zinataanza kutimua vumbi Desemba 8-14, 2018, katika mji wa Sharm El Sheikh, Misri. Bingwa wa mashindano hayo anapata tiketi ya moja kwa moja kucheza Kombe la Dunia la Soka la Ufukweni litakalofanyika Novemba 2019, Paraguay.

MICHEZO YA UFUNGUZI

Malawi v Uganda saa 9:00 Alasiri

Tanzania v Seychelles saa 10:00 jioni