Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) Wallace Karia amepokea kwa masikitiko makubwa kifo cha Mwamuzi wa Kimataifa mstaafu Charles Mchau aliyefariki leo alfajiri kwenye hospitali ya KCMC mkoani Kilimanjaro.

Rais wa TFF Ndugu Karia ametuma salamu za rambirambi kwa msiba huo wa Mchau ambaye pia alikua Kamishna wa mechi za Ligi Kuu ya Tanzania Bara.

“Nimepokea kwa mshtuko mkubwa kifo cha Mchau ambaye alikua bado anautumikia mpira wa miguu,kwa niaba ya TFF natoa pole kwa Ndugu,jamaa na marafiki kwa kuondokewa na mpendwa wao,mwenyezi Mungu awape subira na uvumilivu katika kipindi hiki kigumu na cha majonzi” amesema Rais wa TFF Ndugu Karia.

Amesema Mchau atakumbukwa toka enzi anachezesha mpira wa miguu mpaka kufikia kiwango cha kuchezesha Kimataifa na atakumbukwa kwa kazi yake nzuri wakati akiwa Kamishna wa mechi za Ligi Kuu baada ya kustaafu.

Mungu aiweke roho ya marehemu Charles Mchau mahali pema peponi,Amina.