Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania(TFF) Wallace Karia ameipongeza timu ya Taifa ya Wanawake “Twiga Stars” kwa kurudi na Kombe la Ubingwa wa Jumuiya ya Africa Mashariki kutoka Burundi na kuwataka kudumisha nidhamu mpaka kwenye klabu zao.

Rais wa TFF Ndugu Karia amesema nidhamu ndio msingi wa mafanikio ambayo yanapatikana kwenye mashindano mbalimbali.

Amewataka kwenda na nidhamu hiyo mpaka kwenye ngazi ya klabu ambako wanarudi sasa baada ya kumaliza majukumu ya timu ya Taifa na waepukane na tabia hatarishi.

“Mafanikio mnayoyapata msingi wake ni nidhamu mliyonayo nashukuru sijawahi kusikia nidhamu mbaya katika timu hii,ni vyema pia mkajiepusha na tabia hatarishi” alisema Rais wa TFF Ndugu Karia.

Wakati huohuo Rais wa TFF Ndugu Karia amesema Shirikisho litafanya mpango wa kutafuta mechi za kirafiki na mataifa yenye ushindani ili kuimarisha kikosi hicho cha Twiga Stars.

Amesema mechi hizo zitakuwa dhidi ya mataifa ambayo yamekuwa kikwazo kwa Tanzania.

Wachezaji wa kikosi cha Twiga Stars wameruhusiwa kurudi kwenye timu zao mpaka hapo watakapoitwa kwa maandalizi ya mechi mbalimbali.