Timu ya Taifa ya Vijana U17 “Serengeti Boys kesho Jumatano inashuka dimbani kutupa karata yake nyingine dhidi ya Uganda kwenye mchezo wa Total Afcon utakaochezwa Uwanja wa Taifa.

Mchezo huo utakaoanza saa 11 jioni ni wa pili kwa Serengeti Boys katika mashindano hayo.

Awali Serengeti Boys walifungua pazia la mashindano hayo dhidi ya Nigeria na kukubali kufungwa mabao 4-5.

Mchezo huo wa Kesho ni muhimu kwa Serengeti Boys kupata matokeo ya ushindi ili kuweka hai matumaini yake ya kufanya vizuri katika mashindano hayo pamoja na kuweka hai matumaini ya kucheza Fainali za Kombe la Dunia la Vijana U17

Mchezo mwingine utakaochezwa Kesho ni kati ya Angola na Nigeria utakaoanza saa 8 mchana Uwanja wa Taifa.

Nigeria anaongoza Kundi akiwa na alama 3 sawa na Angola ambaye pia ana alama 3 wakati Tanzania na Uganda hawana alama yoyote.