MSHAMBULIAJI wa timu ya Simba ya Dar es Salaam, John Bocco, amechaguliwa kuwa Mchezaji Bora wa mwezi Aprili wa Ligi Kuu Tanzania Bara (TPL) msimu wa 2018/2019.
Bocco ametwaa tuzo hiyo baada ya kuwashinda wenzake wawili, Emmanuel Okwi wa Simba na Heritier Makambo wa Yanga alioingia nao fainali katika uchambuzi uliofanywa Dar es Salaam wiki hii na Kamati ya Tuzo ya TPL inayotolewa na Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF).
Kwa mwezi huo wa Aprili, Simba ilicheza michezo sita na kushinda mitano na kupoteza mmoja, ambapo Bocco alitoa mchango mkubwa kwa timu yake akifunga mabao matatu na kuifanya Simba ipande hadi nafasi ya pili ikitoka ya tatu iliyokuwepo mwezi uliopita.
Kwa upande wa Makambo yeye aliiongoza Yanga iliyocheza michezo mitano ikishinda mitatu, sare mmoja na kupoteza mmoja, ambapo alifunga mabao matatu na alikuwa na mchango mkubwa katika mafanikio ya Yanga kuendelea kubaki nafasi ya kwanza mwezi huo, wakati Okwi aliyefunga pia mabao matatu alikuwa chachu ya mafanikio ya Simba.
Pia Kamati ya Tuzo, imemchagua Kocha Mkuu wa Simba, Patrick Aussems kuwa Kocha Bora wa mwezi Aprili akiwashinda Kocha Mkuu wa Azam, Abdul Mingange na Kocha Mkuu wa Yanga, Mwinyi Zahera.
Aussems ameifanya Simba iendelee kung’ara katika ligi hiyo, ambapo kwa mwezi huo ilishinda michezo mitano na kupoteza mmoja ikipanda kutoka nafasi ya tatu hadi ya pili, wakati Mingane aliiongoza Azam kushinda michezo mitatu, sare mmoja na kupoteza mmoja, lakini timu hiyo imeshuka kutoka nafasi ya tatu hadi ya pili.
Kwa upande wa Zahera kwa mwezi huo timu yake ilicheza michezo mitano ikishinda mitatu, sare mmoja na kupoteza mchezo mmoja ikiendelea kubaki kileleni mwa msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara inayoshirikisha timu 20. Timu nyingi kwa mwezi huo ukiacha Simba, Yanga na Azam zilicheza mechi chache.
Washindi kila mmoja atazawadiwa sh. 1,000,000 (milioni moja) pamoja na kikombe (trophy) kutoka kwa wadhamini Biko Sports, na kisimbusi kutoka Azam Tv ambao ni wana haki ya matangazo ya Ligi Kuu.