Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) limezindua kampeni maalumu ya Taifa Stars kuelekea katika michezo ya kufuzu AFCON 2021.
Kampeni hiyo inaanzia kwenye mchezo dhidi ya Equatorial Guinea utakaochezwa Ijumaa Novemba 15,2019 Uwanja wa Taifa.
Kampeni hiyo maalumu imepewa jina la “Twenzetu Tena” ikiwa na lengo la kuhamasisha Taifa Stars inayodhaminiwa na bia ya Serengeti kukata tiketi ya kufuzu AFCON kwa mara nyingine.
Katibu Mkuu wa TFF Kidao Wilfred amesema ni jambo kubwa ambalo litasaidia kuongeza hamasa kwa Watanzania na Wachezaji.
Amesema TFF kwa kuzingatia hamasa inayohitajika kiingilio kwenye mchezo dhidi ya Equatorial Guinea kimewekwa cha hali ambayo kila mmoja anaweza kukimudu.
VIP B na C kitakua 5,000 ,Mzunguko 3,000 ambapo tiketi zitaanza kuuzwa mapema.
Naye Meneja Masoko wa Bia za Serengeti Anitha Rwehumbiza amesema Serengeti wataendelea kuunga mkono kama ilivyo kawaida yao akisifia umoja uliopo sasa kuhakikisha Taifa Stars inafanya vizuri.
Amesema Ijumaa katika mchezo huo watahakikisha bia ya Serengeti inapatikana Uwanjani.
Mwenyekiti wa Kamati ya Hamasa Haji Manara amewataka Watanzania kujitokeza kwa wingi kuujaza Uwanja wa Taifa ili kuwaongezea morali Wachezaji.
Nayo Kamati ya Waandishi wa Habari za Michezo kupitia kwa mjumbe wake Charles Abel wameahidi kuibeba Kampeni hiyo kupitia vyombo mbalimbali vya Habari,lengo kubwa ikiwa ni hamasa kuongezeka.
Kwa upande wa Mwenyekiti wa Kundi la Tanzania Taifa Stars Supporters Karigo Godson amewataka Watanzania kushangilia wakati wote wa mchezo na kuifanya taswira ya Uwanja wa Taifa kuwa yenye shangwe kubwa hali itakayowapa Wachezaji morali kubwa ya kupambana zaidi.