Timu ya Tanzania Bara “Kilimanjaro Stars” inatupa karata yake muhimu itakayoamua hatima ya nafasi ya nusu fainali ya Cecafa Challenge.

Kilimanjaro Stars inashuka dimbani KCCA,Lugogo saa 10 jioni kucheza dhidi ya Sudan mchezo wa mwisho Kundi B.

Mchezo huo ni muhimu kwa Kilimanjaro Stars ambao umebeba hatima yake ya kusonga kwenye nusu fainali na kama ikishindwa kuchanga karata zake vizuri itaaga mashindano hayo makubwa ya Ukanda wa Cecafa.

Tayari Kilimanjaro Stars imekusanya alama 3 katika mashindano hayo baada ya kufungwa moja na kushinda mchezo mmoja.

Ilianza kwa kufungwa na Kenya 1-0 katika mchezo wa kwanza kabla ya kupata ushindi wa 1-0 dhidi ya Zanzibar kwa bao pekee la Ditram Nchimbi.

Kilimanjaro Stars inakamata nafasi ya pili Kundi B kwa alama hizo 3 ikiwa nyuma ya Kenya wenye alama 6 ,Zanzibar na Sudan kila mmoja ana alama 1.