Liberia yazinduka na kuwaduwaza Watanzania Uhuru
Mashindano ya U16 ya TFF yanaendelea katika kiwanja cha Uhuru Jijini Dar es Salaam ambapo timu ya Tanzania na Liberia zimeminyana asubuhi ya leo ikiwa ni mchezo wa pili ambapo katika mchezo wa kwanza uliopigwa siku ya Jumanne na Tanzania kuibuka na ushindi wa bao tatu kwa bila.
Mchezo wa leo umeonekana kuwa na tofauti kidogo baada ya Waliberia hao kujiuliza kuwa walikosea wapi na kufanikiwa kubaini makosa na kuweza kuibuka na ushidni wa bao 3-1 matokeo yaliyowaduwaza wenyeji Tanzania kwani Liberia ndio walikuwa wa kwanza kupata bao la mapema kabisa huku wakishambulia kwa kasi ya ajabu na hivyo kupelekea wenyeji kuwachezea Faulo mbaya iliyosababisha kutoka kwa kadi nyekundu ndani ya kipindi hicho cha kwanza tu.
Mpaka timu hizo zinakwenda kwenye mapunziko Liberia walikuwa mbele kwa bao moja kwa bila, bao lilofungwa dakika za mwanzo za mchezo huo.
Kipindi cha pili kilianza huku Tanzania wakionesha kutaka kusawazisha bao hilo na hivyo kupeleka mashambulizi katika upande wa Liberia lakini wakati wenyeji hao wakishambulia Liberia wao walifanya mashambulizi ya kushitukiza na kusababisha kona ambayo ilizaa goli la pili.
Lakini Tanzania nao waliongeza juhudi na kujitutumua vilivyo na kuweza kuzitikisa nyavu za Liberia kwa mara ya kwanza, goli lililofungwa na mchezaji Omary Abbas mwenye jezi namba (10).
Bao hilo halikuwatikisa kabisa Liberia, bali waliendelea kuwa moto zaidi na kuonesha umakini mkubwa katika mchezo huo na hivyo kupelekea goli lingine la tatu dakika ya 40 bao lilopachikwa kimyani na mchezaji jezi namba 17.
Licha ya ushindi mkubwa walioupata Liberia kocha wa timu hiyo amesititiza kwamba timu ya Tanzania ni timu nzuri na wachezaji wake wako makini, na hivyo mchezo wa marudiano wa jumamosi hatarajii kuwa utakuwa mwepesi.
Kwa upande wa kocha wa U16 wa Tanzania Maalim Salehe amesema mchezo ulikuwa mzuri na amewasifu Waliberia kwa ushindi walioupata na kwamba waliweza kuusoma mchezo wa kwanza vizuri na ndio uliopelekea wao kupata ushindi huo, lakini pia amesema timu yake inajiandaa vizuri zaidi kwa mchezo wa marudiano utakaopigwa siku ya jumamosi ya tarehe 14 machi 2020.