Nafasi ya Pili Yazidi Kuwa Ngumu kwa Yanga.

Yanga inazidi kupata changamoto ya kuipata nafasi ya pili katika msimamo wa ligi kuu Bara, hasa baada ya kukubali kutoka sare ya bao 1-1 na Mwadui FC katika mchezo uliopingwa leo katika uwanja wa Taifa, mnamo majira ya saa 1:00 usiku ambapo mechi hiyo ilimalizika kwa Yanga kukubali kuziachia alama mbili ikiwa nyumbani na kujikuta ikipata wakati mgumu katika mbio za kuwanaia nafasi ya pili.

Ni timu ya Yanga ndio ilikuwa ya kwanza kupata bao kupitia kwa kiungo mjanja mjanja na mwenye vyenga vya maudhi Feisali Salum Abdallah a.k.a ‘Feitoto’ mara baada ya krosi nzuri kupigwa na Mrisho Ngassa ‘Anko’ aliyekwenda kupiga kona na kisha kurudishiwa mpira huo aliouachia safi na kumkuta fundi Feitoto aliyeumalizia kwa ulaini kabisa na kuwafanya Yanga kutoka katika kipindi cha kwanza wakiwa mbele kwa bao moja bila.

Kipindi cha pili vijana ‘wavuna madini’ Mwadui waliingia na mbinu mpya na kufanya mashambulizi ya mara kwa mara yenye malengo ya kupata goli; na katika dakika ya 52 tu wakafanikiwa kusawazisha bao na kuzifanya timu hizo kutoka sare ya 1-1.

Sare hiyo ilikuwa na faida kubwa kwa Mwadui na kuwa Mwiba kwa Wanajangwani kutokana na umuhimu wa mchezo huo kwa uopande wao kufuatia mnyukano uliopo katika kuwania nafasi ya pili; kwani timu tatu yaani Azam, Namungo na Yanga wote wanasaka nafasi ya pili.

Mabadiliko aliyoyafanya kocha ya kumtoa Mrisho Ngassa na kumuingiza Erick Kabamba yalisababisha kikosi hicho kupoa na kushindwa kushambulia kama ilivyokuwa awali jambo ambalo lilionekana kuwakera mashabiki wa Yanga na kujikuta wakipiga kelele kumlalamikia kocha wao.

Baada ya bao hilo kurudishwa kocha wa kikosi cha Yanga alikuwa katika wakati mgumu  kutokana na mbinu zote alizozitumia kushindwa kuzaa matunda katika mchezo huo; kwani   matokeo hayo yalionekana kuwa mwiba kwake jambo lililopelekea kocha huyo kushindwa hata kuongea na waandishi wa habari kama ilivyo ada yake.

Vikosi vilivyoshuka uwanjani katika mchezo huo kwa upande wa wenyeji Yanga ni; Metacha Mnata(Golikipa), Juma Abdul, Adeyun Saleh, Lemine Moro, Kelvin Yondani, Said Makapu, Feisal Salum, Mrisho Ngassa, David Molinga, Deusi Kaseke na Ditram Nchimbi. Wale wa akiba walikuwa ni pamoja na; Ramadhani Kabwili (GK), Ally Mtoni, Erick Kabamba, Patrick Sibomana, Yikpe Gislain, Paul Godfrey na Abdul Azizi Makame.

Kwa upande wa Mwadui ni; Mussa Mbisa(GK), Frank John, Yahya Mbegu, Halfan Mbaruku, Agustino Samson,  Mussa Chambega, Wallace Kiyango, Gerad Matius, Raphael Aloba, venance ludovic na Omary Daga; huku wale wa akiba wakiwa ni Mahamoud Amir, Out Joseph, Merckiard Mazellah, Maliki Jafar, Charles Masenga na Enrick Nkosi.

Matokeo mengine ya mechi zilizochezwa leo ni; Mtibwa dhidi ya KMC 1-0,  Namungo 1- Tz Prison 1,  Ndanda FC 0 Mbeya City 1, Ruvu Shooting 0-Singinda United 2, Biashara dhidi ya Coastal Union 1-1 na mchezo wa mwisho ni Kagera Sugar dhidi ya Polisi Tanzania1-1.