Ligi ya Wasichana wa Shule za Msingi U15 Dar es Salaam Yaanza Huku Timu ya Fountain Gate Ikitoa Kichapo Kitakatifu
Michuano ya ligi ya wasichana wa shule za Msingi inayozikutanisha timu nane(8) kutoka shule mbalimbali zilizopo katika mkoa wa Dar es Salaam yamefanyika 15 Agosti, 2020 katika viwanja vya Karume vilivyopo makao makuu ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) ambapo mechi nne zilipigwa.
Kati ya mechi za mapema zilizopigwa viwanjani hapo, ilikuwa ni ya Fountain Gate Academy dhidi ya Gongo la Mboto Jeshini ambapo timu ya Fountain Gate ilifanikiwa kupata ushindi mnono wa jumla ya mabao 6-0 katika mchezo wa awali kabisa uliopigwa majira ya saa 03:30 asubuhi.
Wafungaji wa mabao ya Fountain Gate Academy katika mchezo huo wa awali walikuwa ni; Jacqline Daud Chalula (bao 1), Asia Said Mbuma(1), Prisca Michael Issaya(2), Veneranda Casmir (1) na Mariam Richard(bao 1).
Mchezo mwngine uliopigwa mapema pia ulikuwa ni kati ya Zimbili na Mtoni Kijichi; mchezo amabao ulimalizika kwa timu hizo kutoshana nguvu kwa kupata suluhu ya bila kufungana. Timu zilizoanza mashindano haya ndizo zilizokuwa katika kundi A.
Mechi za kundi B zilifuatia ambapo zilizikutanisha timu kati ya Minazini dhidi ya Kawe B; mchezo uliomalizika kwa Minazini kuibuka na ushindi wa bao 3-0, magoli ambayo yote yalifungwa na Rahma Abduli ambaye pia ndiye mchezaji pekee aliyeweza kupata hati triki katika mechi za uzinduzi wa michuano hiyo.
Mechi nyingine za kundi B zilikuwa ni; kati ya Joyland dhidi ya Gezaulole ambapo Joyland ilifanikiwa kuibuka na ushindi wa bao 1-0.
Baadhi ya makocha wa timu hizo walikuwa na maoni tofauti tofauti kuhusiana na mechi hizo ambapo kocha wa Fountain Gate Academy Martha Samoya Magese alisema kuwa kikosi chake kimecheza vizuri na kilifuata maelekezo kiliyoyapata kutoka katika benchi lake la ufundi. Kocha huyo aliongeza kuwa kikosi chake kilikuwa na makosa madogomadogo licha ya ushindi mkubwa kilichoupata huku akiahidi kwenda kuyafanyia kazi mapungufu aliyoyaona ili kuweza kufanya vizuri zaidi katika mechi zitakazo fuata.
Kwa upande wa kocha wa timu ya Gongolamboto Jeshini mwalimu Antonia Jeremiah yeye alieeleza bayana kuwa kikosi chake kilipoteza umakini na hivyo kusababisha kupata matokeo hayo yasiyoridhisha. Hata hivyo, kocha huyo aliahidi kwenda kuyafanyia kazi makosa hayo yaliyojitokeza kwenye mchezo wake wa kwanza ili kuweza kujenga kikosi imara na chenye ushindani maradufu.
Naye kocha wa timu ya Minazini, Clara Vicent Samuel baada ya kuibuka na ushindi wa bao 3-0 dhidi ya Kawe ‘B’ alimshukuru Mungu kwa matokeo hayo aliyoyapata huku akidai kuwa amejipanga kuchukua ubingwa wa mashindano hayo na kwamba matokeo hayo ilikuwa ni salamu tu kabla ya mazungumzo kamili.
Wakati kocha wa Kawe B Samson Sanyagwe naye pia akisema kuwa kikosi chake kilishindwa kuzitumia vema nafasi zilizopatikana hivyo kudai kuwa amekwisha kuyaona mapungufu na kwamba atafanyia kazi ili katika michezo mengine kikosi chake kiweze pata matokeo mazuri.
Mashidano hayo ya ligi ya wasichana kutoka shule za msingi mbalimbali za mkoa wa Dar es Salaam yameandaliwa na TFF kwa utaratibu wa CAF; tayari yamekwisha kuanza rasmi na yataandelea tena kutimua vumbi katika viwanja vya Karume kila siku ya jumamosi mpaka hapo yatakapo fikia mwisho.
Lengo kuu la mashindano haya ni kujaribu kuibua vipaji vya watoto na vijana wenye umri chini ya miaka 15 kuweza kuvifundisha na kuviendeleza vipaji hivi ili visije vikapotea bure mtaani.
Na hii yote ni kwa ajili ya kutekeleza mpango maalum wa maendeleo wa soka la wanawake na vijana nchini Tanzania.