Lameck Nyambaya Akabidhi Mpira 50 kwa Kanda ya Dar es Salaam

Mjumbe wa kamati tendaji ya kanda ya Dar es salaam Lameck Nyambaya amekutana na waandishi wa habari tarehe 10 Septemba, 2020 katika ukumbi wa mikutano wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Nchini Tanzania TFF, uliopo Karume jijini Dar es salaam na kukabidhi mipira kwa wilaya tano za mkoa wa Dar es salaam.

Tukio hilo lilishuhudiwa na Rais wa shirikisho la mpira wa miguu nchini Tanzania Wallace Karia na makamu wa kwanza wa Rais wa shirikisho Athumani Nyamlani na wote kwa pamoja wametoa shukurani za dhati kwa mjumbe huyo kwa kujitoa kimasomaso kukuza na kuinua soka hapa nchini kwani mipira hiyo itaenda kusaidia ligi mbalimbali hapa Dar es salaam.

Aidha Rais Karia amempongeza mjumbe huyo kwa kujitoa katika jambo hili kwani halijawai kufanywa na kiongozi yoyote wa kanda hiyo ya Dar es Salaam. Rais Karia aliwaomba viongozi wengine kuchukua kitendo hicho kama hamasa ya kuongeza juhudi katika kukuza soka nchini na kumalizia kwa kusema kuwa viongozi wote wana mchango katika kila wanacho kifanya hivyo anaheshimu na kutambua juhudi zao.

“Mipira hii imekuja sehemu sahihi katika kanda hii ya Dar es salaam kwa sababu ni moja ya kanda ambayo ina timu nyingi zinazoundwa na wilaya tano hivyo mipira hii itaenda moja kwa moja kutumika katika ligi za ndani ya mkoa na itapunguza kwa kiasi fulani changamoto za ukosefu wa mipira katika kanda ya Dar es salaam.” Alisema Rais Karia kwa furaha.

Sambamba na hayo mwakilishi wa wilaya zote tano mwenyekiti wa chama cha mpira wa miguu wilaya ya Temeke mkoa wa kimpira ndugu Peter Steven Mhinzi amemshukuru sana ndugu Nyambaya kwa kujitoa kwake katika jambo hili la kujitolea vifaa hivi kwa upande wao kama viongozi wa mpira vimekuja katika wakati sahihi kwani ligi zina uhitaji mkubwa wa mpira.

Wilaya zilizo pewa mipira hiyo ni; Ilala, Kinondoni,
Temeke, Kigamboni na Ubungo na kila wilaya imekabidhiwa mipira 50.