Waamuzi 120 wa Daraja la Pili Wahitimu Kozi ya Kuongeza Uwezo kwa Mkapa, Dar es Salaam.

Shirikisho la Mpira wa Miguu nchini Tanzania (TFF) limefunga rasmi mafunzo ya waamuzi ligi daraja la pili hii leo 30 Septemba, 2020 katika uwanja wa Mkapa jijini Dar es salaam.

Mafunzo hayo yenye mjumuisho wa waamuzi 120 kutoka sehemu mbalimbali ndani ya Tanzania yalianza tarehe 19 Septemba katika kiwanja cha Benjamin Mkapa yakiwa na lengo kuu la kuona ujuzi waliokuwa nao awali na kuwaendeleza zaidi katika nyanja zote za kutafsiri sheria za mpira na kuweka miili yao katika hali ya utimamu.

Aidha mwenyekiti wa kamati ya waamuzi yaTFF, Soud Abdi amewapongeza waamuzi kwa kuonesha utayari wa kutaka kufahamu mambo mapya na kupenda kujifunza kwa muda wote wa mafunzo na amewataka waamuzi washiriki kuchukulia mafunzo hayo kama sehemu muhimu kwao ili kukuza mpira wetu nchini.

Sambamba na hayo Soud Abdi alisema “Nia kubwa ya mafunzo haya ni kupata vijana wapya katika ngazi za juu za wamuzi hivyo tumefanya mafunzo haya kuangalia kama tunaweza kuwatumia waamuzi hawa katika ligi mbalimbali huko mikoani lakini pia tunataka kuimarisha uwezo wao na kuukuza zaidi ili mbeleni tupate kuona wanapanda madaraja ya juu zaidi ya hapa’’ alisema Soud.

Kwa upande wa washiriki nao wale waliopata nafasi ya kutoa maoni yao walisema:
‘’Mafunzo haya ni mazuri kwa upande wetu kwani yanatupa uwezo wa kujipima wapi tupo na nini tufanyie kazi. Vilevile, yanatukutanisha na waamuzi wenzetu kutoka sehemu tofauti tofauti hapa Tanzania; hivyo tunaushukuru sana uongozi mzima wa shirikisho la mpira wa miguu Tanzania ulio chini ya Rais Wallace Karia na Katibu Mkuu Kidao Wilfred kwa kuwezesha mafunzo haya’’