Makamu wa Kwanza wa Rais TFF  Atoa Neno kwa Washiriki wa Kozi na Vilabu vya Mpira

Kozi ya uongozi na usimamizi wa soka kwa wanawake imefunguliwa rasmi jijini Arusha tarehe 28 septemba 2020 na Makamu wa Kwanza wa Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania ndugu, Athumani Nyamlani.

Akifungua kozi hiyo  alisema kwamba anashukuru kwa mapokezi mazuri aliyoyapata kutoka kwa wenyeji,  na kwa hakika anaona mabadiliko makubwa yatakayopatikana kupitia kozi hizo zinazotolewa kwa wanawake  kutokana na mwitikio mkubwa uliopo na hamasa ambayo ameiona kutoka kwa washiriki ambapo wote walionekana kuwa na bashasha na utayari wa kuyapokea mafuzo hayo.

Ndugu Nyamlani alikazia kwamba TFF ni waumini wa kwenda na wakati hivyo kwa hivi sasa katika mambo ya uongozi wanawekeza zaidi kwa wanawake wakiwa na matumaini makubwa ya uwezo wao katika uongozi; hivyo basi,  anaamini uwekezaji huo utakuwa na matokeo chanya hasa ukizingatia kuwa katika soka la wanawake ndiko mafanikio makubwa yamekuwa yakipatikana na hata katika upande wa mataji wanawake wanaongoza ukilinganisha na soka la wanaume.

Mbali na hayo  alitoa rai kwa vilabu na vyama vya mpira kupenda kuhudhuria kozi mbalimbali za uongozi ama nyingine zenye maudhui tofauti tofauti yanayohusiana na mpira wa miguu; kwani hivi sasa mpira umebadilika kutoka kwenye mpira wa fikra na kuwa mpira wa sayansi hivyo unaitaji ujuzi wa ziada ili mtu aweze kulandana na mazingira yaliyopo.

Makamu Nyamlani alihitimisha kwa kusema kuwa huu ni wakati wao kuchangamkia fursa na kuacha kufanya mambo au kuongoza vitu kimazoea; na katika suala la kuongezea ujuzi wasibague aina ya wakufunzi, kwani kuna kasumba ya watu kuamini kwamba wakufunzi wa nje ndio bora zaidi kuliko wa wandani jambo ambalo halina ukweli wowote.

Mafunzo hayo yanatarajiwa kumalizika mapema mwezi Oktoba, 2020 na baadae  kuendelea katika mikoa mingine ya Tanzania Bara na Visiwani.