Yanga Yaendelea Kuvuna Pointi  Yapiga Coastal Union kwa Mkapa

Mchezo kati ya Yanga na Coastal Union ya Tanga umemalizika kwa timu ya Wanajangwani kuibuka na ushindi mnono wa bao 3-0; na kuwafanya Wagosi wa Kaya kutoka uwanjani wakiwa vichwa chini.

Mtanange huo uliopigwa majira ya saa 1:00 usiku kwenye uwanja wa Mkapa ulikuwa na vionjo vyake huku timu hizo zikitoshana nguvu katika kipindi cha kwanza ambapo hakuna timu iliyoweza kuzifumania nyavu za mwenzeka. Katika kipindi cha kwanza timu zote zilionekana kucheza kwa tahadhali kubwa na nidhamu ya hali ya juu ikiwa ni moja ya mbinu za kutoruhusu kufungwa mapema.

Kipindi cha pili kilianza huku Yanga wakionekana kurejea na kasi mpya baada ya kocha wa kikosi hicho kufanya mabadiliko kwa kumtoa Zawaid Mauya na kuingia Haruna Niyonzima © wakati huo huo Kibwana Shomari naye akimpisha Deusi Kaseke; wachezaji hao walileta uhai na kuifanya timu kupeleka mashambulizi ya mara kwa mara kwenye lango la wapinzani wao.

Magoli yote ya Young Africans katika kipindi cha pili ambapo mnamo dakika ya 49  Carlos  Sterio alipachika bao la kuongoza kabla ya Haruna Niyonzima kutikisa nyavu kunako dakika ya 52 huku bao la tatu na la mwisho likifungwa mnamo dakika ya 64 na kuwafanya wananchi kutoka na ushindi mkubwa wa bao 3-0 tangu waianze ligi ya Vodacom msimu wa 2020/2021.

Kocha wa Yanga Krmpotic Zlatco alisema kuwa kikosi chake kilicheza vizuri licha kuwepo kwa makosa ya hapa na pale.  Kocha huyo aliongeza kuwa baadhi ya wachezaji hawakufanya vema huku akimtolea mfano beki wa kushoto Adeyun Salehe kuwa alikuwa akifanya makosa mengi katika eneo lake. Hata hivyo, kocha Zlatco alisema kuwa anampango wa kuifanya timu hiyo ya wananchi kucheza vizuri zaidi kuliko inavyofanya sasa kwani kikosi chake bado hakijapata muunganiko wa kutosha kuleta ushindani unaotakiwa.

Wakati kocha mkuu wa kikosi cha Wagosi wa Kaya Juma Mgunda  yeye akitanabaisha ya kwamba kikosi chake kilikuwa kikicheza kwa tahadhali kwa kuwa kilijua fika kuwa timu ya Yanga ni timu kubwa na yenye uwezo wa kufanya lolote wakati wowote. Kocha Mgunda alieleza kuwa kikosi chake kilifanya makosa kadhaa ambayo yalipelekea kupoteza mchezo huo.

Aidha Mgunda aliongeza kuwa kwa sasa bado anakijenga kikosi chake kutokana na kuuza wachezaji wake wengi akiwemo Bakari Nondo Mwanyeto ambaye kwa sasa anakipiga kwa wanajangwani hao.

Vikosi vilivyocheza katika mechi hiyo kwa upande wa wenyeji Young Africans walikuwa na Metacha Mnata (GK) Kibwana Shomari, Adeyun Salehe, Bakari Nondo Mwamyeto, Lamine Moro, Mkoko Tonombe, Tuisila Kisinda, Feisal Salum (Feitoto), Zawadi Mauya, Yacoub Songne na Carlos Sterio; huku wale wa akiba wakiwa ni Farouk Shikalo (GK), Abdulazizi Makame, Deusi Kaseke, Said Juma Makapu, Haruna Akizimana Niyonzima na Ditram Nchimbi.

Kwa upande wa kikosi cha Coastal Union kulikuwa na; Abubakari Abasi (GK), Hassan Jafari, Hance Masoud, Seif Yona, Peter Mwangosi, Salum Ally, Abdul Seleman, Mtenje Juma, Mudathir Said, Issa Abushehe,  Hamad Rajabu wakati wachezaji wa akiba walikuwa ni pamoja na; Diey Hassan (GK), Ayoub Masoud, Mwinyi Said, Muhsin Malima, Raizin Hafidh, Yusuph Abasi na Rashid Mohamed.

Kwa matokeo ya mchezo huo Yanga sasa wanakuwa na alama 13 baada ya kucheza mechi tano huku watani wao Simba wakiwa na alama zao 10 baada ya kushuka dimbani mara nne. Kikosi cha Msimbazi kitashuka kesho ndimbani kuminyana na JKT Tanzania; mchezo utakao pigwa katika dimba la Jamhuri Makao Makuu ya Serikali Dodoma.