Serengeti Kumwaga Mabilioni kwa Timu ya Taifa Stars
Bia ya Serengeti Premium Larger (SPL) imeingia makubaliano ya kusaini mkataba mpya na Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania TFF katika hafla iliyofanyika Octoba 6 2020 katika hoteli ya Serena iliyopo katikati ya Jijini Dar es Salaam.
Mkataba huo mpya uliogharimu shilingi bilioni 3 za kitanzania umesainiwa baada ya ule mkataba wa awali uliosainiwa mwaka 2017 kufikia ukomo katikati ya mwaka huu, hivyo basi mkataba huo una lengo la kuipa timu ya taifa ya ‘Taifa Stars’ udhamini kwa kipindi cha miaka mitatu mfululizo.
Mkurugenzi mtendaji wa SBL ndugu, Mark Ocitti alisema kuwa Bia ya Serengeti Premium Lager ni mdau mkubwa wa michezo hapa nchini na kuongeza kuwa imekuwa ikijivunia katika suala zima la kuwaunganisha watanzania kupitia michezo, na kuongeza kwamba kama kampuni wanatambua na kufahamu umuhimu wa michezo katika kuleta maendeleo ya kijamii na kiuchumi kwa mtu mmoja mmoja na taifa kwa ujumla.
Ndugu Ocitti akazidi kukazia kuwa kuipa Taifa Stars udhamini siyo tu wanachangia katika maendeleo ya michezo bali pia wanachangia kuukuza mchezo wa mpira wa miguu ambao umekuwa mchezo pendwa na uliojizolea mashabiki lukuki duniani ikiwa ni pamoja na Tanzania pia. Lakini msukumo mkubwa uliowafanya Serengeti kuongeza fedha katika udhamini huu mpya ni matokeo ya kuridhishwa na maendeleo pamoja na mafanikio makubwa ya timu ya taifa kwa kipindi cha awali cha udhamini wake; vile vile usimamizi madhubuti wa matumizi ya fedha na utekelezaji wa mipango mikakati ya kuendeleza mpira kwa ujumla inayofanywa na uongozi wa TFF uliopo madarakani kwa sasa.
Naye Rais wa TFF Wallace Karia aliwashukuru kampuni ya Serengeti kwa kukubali kuendeleza udhamini wao kwa timu ya Taifa ya Tanzania na kukiri kwamba katika kipindi chote cha udhamini timu imepata mafanikio mengi kuamzia kushiriki mashindano ya CHAN na mashindano makubwa ya AFCON. Hata hivyo, aliishukuru serikali ya Tanzania iliyo chini ya uongozi wa Mh. Rais Daktari John Pombe Magufuli kwa kuwa mstari wa mbele katika kuiinua timu ya taifa kwa kuweka mazingira rafiki kwa shughuli za michezo kufanyika bila changamoto na kutoa misaada pale inapohitajika, zaidi na zaidi katika kuhamasisha suala zima la uzalendo kwa timu ya Taifa stars.
Katibu Mkuu wa TFF Kidao Wilfred naye alisema kwamba kupata udhamini ni jambo kubwa kwani kuiendesha timu ya Taifa sio jambo jepesi kama watu wengi wanavyofikiri, hivyo anatoa wito kwa wadau wengine kuzidi kuwekeza katika timu hii ili kulipa shirikisho unafuu wa kuweza kuendelea na miradi mingine mbalimbali katika kustawisha sekta hii ya michezo.
Kocha Mkuu wa kikosi cha Taifa Stars, Etienne Ndayiragije alitoa pongezi kwa Serengeti na TFF pia kwa kufikia makubaliano hayo ya kuongeza mkataba mpya wa miaka mitatu; huku akisema kuwa jambo lililofanyika ni zuri na lina tija katika kuleta matokeo chanya kwa timu ya Taifa. Alitoa kauli ya matumaini kuwa sasa wachezaji wake watakuwa na morali wa kucheza kwa kuwa wanauhakika zaidi ya kuimarika kwa mazingira ya mpira. Kocha huyo alitoa wito kwa mashabiki kujitokeza kwa wingi siku ya mechi ili kuongeza hamasa ya mchezo na kuwatia nguvu wachezaji siku hiyo.
Kwa upande wa nahodha msaidizi wa timu ya taifa John Bocco alisema kuwa anaipongeza TFF kwa kazi kubwa wanayoifanya; kwani soka la Tanzania hivi sasa limebadilika na limekuwa na mvuto wa aina yake ukilinganisha na hali ilivyokua kwa siku za nyuma, lakini pia aliwashukuru Serengeti kwa udhamini wao kwa mara nyingine kwani anaamini kupitia udhamini huu Timu ya taifa itazidi kufanya vizuri .
Nahodha Bocco akatumia nafasi hiyo kuwaomba watanzania wote kufika katika uwanja wa Mkapa siku ya tarehe 11 ya mwezi Octoba katika mechi ya kirafiki dhidi ya timu ya Taifa ya Burudi, na kuwaahidi watanzania kutegemea mambo mazuri kutoka kwa timu yao na kwamba hawatawaangusha kwani wamejipanga vizuri na wamefanya maandalizi ya kutosha.