Azam yaibuka na ushindi mnono dhidi ya Ihefu

Timu ya Azam FC imefanikiwa kupunguza pengo la alama tisa kutoka kwa vinara wa ligi kuu; Young Africans na kubakiza alama sita pekee baada ya kupata ushindi kwenye Mchezo uliopigwa majira ya saa 1:00 usiku katika uwanja wa Azam Complex Chamazi dhidi ya Ihefu baada ya kushinda bao 3-0.

Ni dakika tisa pekee ziliwatosha Azam kuweza kuandika bao la kuongoza kupitia kwa mshambuliaji wake Idd Selemani Nado (jezi 23) aliyeunganisha pasi safi iliyopigwa na Abdul Omary (jezi 02) na kuwafanya Azam kwenda kwenye mapunziko  ikiwa na bao moja.

Baada ya timu hizo kurejea kwenye kipindi cha pili Azam FC waliingia kwa kasi zaidi huku wakitaka kupachika bao jingine kabla ya Ihefu hawajachangamka na kuweza kusawazisha bao hilo ambalo lilipatikana  katika kipindi cha kwanza.

Kunako dakika ya  51 kipindi cha pili Azam walifanikiwa kuongeza bao la pili kupitia kwa Ayubu Lyanga (jezi 7) aliyepiga shuti kali kwa guu lake la kushoto lililokwamisha mpira ule kimyani na kumfanya Mlinda mlango wa Ihefu  Deogratus Munishi (Dida) kushindwa kuokoa mpira kabla ya Idd Nado kurejea tena kambani na kupachika bao la tatu, huku bao hilo likiwa ni la pili kwake katika Mchezo huo.

Bao hilo lililofungwa katika muda wa dakika za lala salama lilihitimisha idadi ya magoli nakuufanya mchezo huo kumalizika kwa Azam FC kuibuka na ushindi huo mnono wa bao 3-0.

Kocha msaidizi wa Azam FC Vivier Bahati aliuzungumzia mchezo huo kuwa ulikuwa mzuri licha ya wachezaji kupoteza nafasi nyingi anashukuru kwa kuwa wameshinda. Aliongeza kuwa mchezo huo ulikuwa ni muhimu kwa wao kushinda kutokana na uhitaji mkubwa wa alama tatu waliokuwa nao. Kwani waliamini kuwa  kufanikiwa kupata alama kutakuwa kumewasogeza na kupunguza pengo lililokuwepo kati yao na vinara wa ligi hiyo Young Africans ambao wana alama 50 sasa.

Kwa upande wake kocha wa timu ya Ihefu Zuberi Katwila yeye alisema kuwa amekubali kwamba mchezo huo wamepoteza kutokana na kuzidiwa kidogo na kukosekana kwa umakini na ufanisi wa mchezaji mmoja mmoja ambao ulipelekea kikosi chake kuadhibiwa. Hata hivyo, kocha huyo aliongeza kwa kusema kuwa anaamini licha ya kubakiza mechi kumi pekee, ligi bado inaendelea na kwamba bado wananafasi ya kupambana na kupata matokeo yatakayowawezesha kubaki katika ligi kuku Bara msimu ujao wa 2021/2022.

Naye msemaji wa Klabu ya Azam FC Zaka Zakazi alisema kuwa matokeo hayo ni muhimu kwao na yanazidi kuwaweka katika nafasi nzuri ya kuendelea kuusaka ubingwa wa ligi hiyo ya Vodacom Tanzania Bara.

Kwa matokeo hayo Azam FC anazidi kusalia kwenye nafasi yake ya 3 akiwa na alama 44 akiwa ameshuka dimbani mara 24 huku akiachwa alama mbili na Simba ambaye ana alama 46 baada ya kushuka dimbani mara 20 wakati Young Africans wao wakiwa mbele kwa alama 50 baada ya kucheza michezo 23.