Kikosi Stars Kipo Tayari Kuikabili Harambee Stars ya Kenya

Timu ya Taifa ya Tanzania “Taifa Stars” imefanya mazoezi yake ya mwisho katika uwanja wa Taifa wa Kenya kwa ajili ya kujiandaa na mchezo wake wa kwanza wa kirafiki dhidi ya Harambee Stars ya Kenya hapo tarehe 15 Machi, 2021.

Kikosi hicho kinatarajiwa kushuka uwanjani kupimana nguvu na wenyeji wao Harambee Stars ikiwa ni sehemu ya kujiweka sawa kuelekea michezo yake miwili ya kufuzu kushiriki michuano ya AFCON ya mwaka 2022. Michezo itakayoikutanisha Taifa Stars dhidi ya Equatorial Guinea na Libya Machi, 2021.

Kocha wa kikosi hicho cha “Taifa Stars’ Kim Poulsen akiwa katika mazoezi hayo ya mwisho kabla ya mchezo huo wa kesho (leo) alisema kuwa timu yake imeendelea vizuri na mazoezi ya namna ya kutoa na kupokea pasi ikiwa ni sehemu muhimu katika soka; na kwamaba anaamini kuwa mchezo utakuwa mzuri kutokana na utimamu wa wachezaji wote alionao kufuatia uwezo mzuri waliouonesha mazoezini.

Kocha Kim aliongeza kuwa anamatumaini makubwa na vijana wake kutokana na maandalizi ya nguvu waliyoyafanya kwa muda wa yapata siku sita; na kwamba kikosi hicho kipo tayari kwa ajili ya mchezo huo wa kwanza wa kirafiki wa kimataifa unaotarajiwa kupigwa hapo (15/03/2021) nchini Kenya.

Katika hatua nyingine Serikali ya Tanzania imesema kuwa iko tayari kutoa ushirikiano wa hali na mali kwa timu ya Tanzania kuhakikisha kuwa kila jambo linakwenda sawa kwa muda wa siku zote ambazo timu ya Tanzania Stars itakapokuwa kambini kabla ya kuianza safari ya Equatorial Guinea mwishoni mwa Machi, 2021.

Hayo aliyasema Balozi Dkt. John Simbachawene wa Tanzania inchini Kenya alipokuwa akiipokea Taifa Stars na uongozi mzima ulioambatana na timu kwa ajili ya kuweka kambi na kucheza michezo miwili ya kirafiki ambapo mchezo wa kwanza utapigwa tarehe 15 Machi, 2021 huku ule wa pili ukitarajiwa kupigwa 18 Machi.

Akizungumza na wachezaji na viongozi hao Balozi Simbachawene alisema kuwa serikali inafurahi kuona timu inafanya vizuri na yeye akiwa mtanzania anafuraha zaidi kukutana na watanzania waliokwenda kwa ajili ya kuliwakilisha Taifa la Tanzania na kwamba anamatumaini makubwa na timu hiyo pamoja na uongozi ulioambatana nayo kuwa utaleta matokeo chanya.

Aidha aliongeza kwa kusema kuwa licha ya kuzuiwa kwa mashabiki kuingia uwanjani, bado yeye pamoja na maofisa wake watakwenda kuwashangilia ili kuongeza nguvu yao kwa timu ya nyumbani huku akielezea kuhusu hali ya mazingira ya Kenya kuwa haitofautiani sana na Tanzania, hivyo hana shaka kuhusu hilo.

Baada ya mazoezi ya mwisho mchezaji wa kikosi cha Stars Himid Mao Mkami (07) alizungumza kwa niaba ya wachezaji waliotangulia nchini Kenya, kiungo huyo mkabaji wa Tanzania alisema kuwa wachazaji wote wako tayari na kwamba mwalimu amekwisha maliza kazi yake ya kuwaelekeza kilichobakia ni wao tu kwenda kuyatumia maarifa waliyopewa ili kuweza kupata matokeo.

Naye golikipa mgongwe na nahodha msaidizi wa kikosi hicho cha Stars Juma Kaseja aliongeza kwa kusema kuwa wanaishukuru serikali ya Tanzania kwa sapoti inayowapa katika kila hatua huku akiahidi kuwa yeye na wachezaji wenzake wote waliotangulia na watakaofuata watakwenda kupambana ili kupata ushindi na kuweza kuipeperusha vema bendera ya nchi.