Stars Mguu Sawa kwa Harambee, Baada ya Kujiuliza Maswali Ilikuaje…?

Timu ya Taifa ya Tanzania, ‘Taifa Stars’ imefanya maandalizi kuelekea mchezo wake wa pili wa kirafiki utakaopigwa tarehe 18 Machi,2021 dhidi ya Harambee ya Kenya.

Timu hiyo imefanya mazoezi hayo huku ikiwa na kumbukumbu ya kupoteza mchezo wake wa kwanza iliyocheza tarehe 15 Machi, 2021 dhidi ya Harambee hiyo hiyo ya Kenya kwenye uwanja wa Nyayo uliopo jijini Nairobi; baada ya mchezo huo kumalizika kwa Tanzania kufungwa bao 2-1.

Akizungumzia maandalizi yao kuelekea  mchezo huo  utakao pigwa hapo kesho, kocha msaidizi wa kikosi hicho cha Stars Juma Mgunda alisema kuwa mchezo huo wa kesho ni muhimu kwa kikosi chao na kwamba utawapa tathimini nzuri kujua kiwango kilichofikiwa na wachezaji wao katika kujiandaa na michezo miwili ya kufuzu kushiriki AFCON ambayo inatarajiwa kuchezwa Machi, 2021 dhidi ya Equatorial Guinea na Libya.

Akitoa maelezo zaidi kuhusu hali ya wachezaji kocha huyo alibainisha kuwa wachezaji wote waliokwisha kuripoti wako vizuri na wameendelea na mazoezi yao vema na kwamba wako tayari kwa ajili ya mchezo wao wa kirafiki wa kimataifa pamoja na ile miwili ya kufuzu kushiriki AFCON 2022.

Aidha kocha Mgunda aliongeza kwa kusema kuwa wachazaji wote walioitwa katika kikosi wanapaswa kuitumia vema nafasi hiyo adhimu ili kujitangaza na kujihakikishia nafasi ikiwa pia ni pamoja na kulipambania taifa; kwani wao wanajukumu kubwa la kutambua umuhimu wa michezo hiyo kwa taifa lao.

Naye nahodha wa kikosi hicho Juma Kaseja alisema kuwa wamejiandaa vizuri na kwamba wanaingia kwenye mchezo huo huku wakikumbuka kuwa mchezo wao wa kwanza walipoteza dhidi ya hao hao Harambee Stars, sasa anaimani kuwa walimu walishafanyia marekebisho na kwamba sasa wako sawa kwa ajili ya kulipambania taifa lao kwa hali na moyo wao wote.

Kaseja aliongeza kuwa  anafahamu kwamba wao kama wachezaji wakongwe wananafasi pia ya kuwaelekeza na kuwasaidia wadogo zao ambao ndio wameitwa kwa mara ya kwanza na waale wanao pungukiwa uzoefu. Hivyo, kwa mchanganyiko uliopo kwenye timu ya awamu hii anaamini kuwa wataweza kuwasaidia kuweza kufanya vizuri zaidi; japokuwa haitakuwa rahisi kuifunga Harambee Stars lakini wanakwenda kupambana kwa kila hali ili waweze fanya vizuri katika mchezo huo na hiyo miwili dhidi ya Equatorial Guinea na Libya.

Taifa Stars itaingia kesho uwanjani kuvaana na Harambee Stars ya Kenya baada ya mchezo wake wa kwanza uliopigwa kwenye uwanja wa Nyayo Nairobi 15 Machi,2021 kumalizika kwa Stars kupoteza kwa bao 2-1; wachezaji na benchi la ufundi liko tayari kwa kupambana hiyo kesho kwenye mchezo huo wa kirafiki wa kimataifa.