SIMBA YAREJEA KWA KISHINDO VPL, YAIPIGA MTIBWA 5

Timu ya Simba ya Dar es salaam imerejea kwa kishindo kunako Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania VPL ikiibuka na ushindi wa mabao 5-0 kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa.

Simba walianza kuandika bao lao la kwanza kupitia kwa Clatous Chama dakika ya 9 kabla ya kuongeza mengine mawili kupitia kwa Larry Bwalya na Meddie Kagere.

Mpaka timu hizo zinakwenda mapumziko Simba alikuwa akiongoza kwa mabao 3-0.

Kipindi cha pili kilianza kwa Mtibwa kutaka kusawazisha lakini walikuwa ni Simba walioongeza bao la nne katika dakika ya 51 lililofungwa na Kagere na Luis Miquissonne akafunga bao la tano na kuufanya mchezo huo kumalizika kwa Simba kurejea kwa kishindo katika VPL kwa ushindi wa mabao hayo matano.

Kocha wa Simba Gomes Da Rosa, ameridhishwa na kiwango kilichooneshwa na wachezaji wake huku akiwapongeza kwa matokeo hayo mazuri na kuahidi kuendelea kuyafanyia kazi makosa ili kukifanya kikosi hicho kuwa imara zaidi katika harakati za kuutetea ubingwa wao.

Kocha msaidizi wa Mtibwa Sugar Sudi Slim amesema kikosi chake kimeathiriwa na mfungo wa mwezi mtukufu wa Ramadhani kutokana na idadi kubwa ya wachezaji wake kucheza huku wakiwa wapo kwenye mfungo.

Ameongeza kuwa mbali ya mfungo lakini pia wamecheza na Simba yenye kikosi kizuri.

Kwa upande wa Meddie Kagere aliyepachika mabao mawili amesema kila mchezaji anayecheza nafasi ya ushambuliaji hujisikia furaha anapofunga magoli mengi huku nahodha wa Mtibwa Sugar Issa Rashid, akisema wamepoteza mchezo huo lakini bado wananaendelea kupambana ili waweze kusalia kwenye ligi licha ya ugumu wanaokabiliana nao.

Matokeo hayo yanaifanya Simba kufikisha alama 49, na kupanda kwenye nafasi ya pili iliyokuwa inashikiliwa na Azam FC