Timu za Nyaishozi SC ya Kagera na Baga Friends ya Pwani zimekata tiketi ya kucheza nusu fainali ya Ligi ya Mabingwa wa Mikoa (RCL) 2021 kutoka Kundi B.

Nyaishozi na Baga Friends zimekata tiketi hiyo baada ya leo kukamilisha hatua ya makundi kwa kukutana kwenye mchezo uliomalizika kwa Nyaishozi kuibuka na ushindi wa mabao 3-1 kwenye uwanja wa Ilulu,Lindi.

Mabao ya Nyaishozi yalipatikana kupitia kwa Idris Stambuli dakika ya 34 ambalo lilidumu mpaka mapumziko.

Katika kipindi cha pili Nyaishozi wakaongeza mabao mengine mawili kupitia kwa Eggy Senari dakika ya 58 na Idris Stambuli akafunga bao la 3 dakika ya 78 huku Baga Friends wakipata bao la kufutia machozi kupitia kwa Hassan Luyaya dakika ya 93 na kufanya mchezo kumalizika kwa Nyaishozi kupata ushindi wa mabao 3-1.

Licha ya kipigo hicho Baga Friends wameungana na Nyaishozi kucheza nusu fainali wakati kundi A timu za Temeke Squad ya Dar es salaam na Copco Vererans ya Mwanza zimefuzu katika hatua hiyo.

Michezo ya nusu fainali itachezwa Aprili 23 Uwanja wa Ilulu, Lindi ambapo Temeke Squad watacheza dhidi ya Baga Friends saa 10 jioni ukitanguliwa na mchezo wa Nyaishozi SC na Copco Veterans saa 8 mchana.