Mwamuzi Emmanuel Mwandembwa wa Arusha atachezesha mchezo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania (VPL) utakaochezwa Jumamosi Mei 8 Uwanja wa Benjamin Mkapa.

Mwandembwa atasaidiwa na mwamuzi msaidizi namba moja Frank Komba wa Dar es Salaam, mwamuzi msaidizi namba mbili Hamdani Saidi kutokea Mtwara na mwamuzi wa akiba Ramadhani Kayoko wa Dar es salaam.

Mwenyekiti wa kamati ya waamuzi, Soud Abdi ametoa ufafanuzi wa kutumika waamuzi wanne tofauti na ilivyozoeleka kutumika Waamuzi 6, ambapo amesema inatokana na maelekezo ya Shirikisho la Mpira wa miguu Afrika (CAF) ya kufanyika kwa mabadiliko yanayomuwezesha mwamuzi wa katikati kufikia uwezo wa juu wa uchezeshaji.

Amesema kuna maeneo ambayo yanamuhitaji mwamuzi wa katikati kuwepo ambayo kimsingi yanampunguzia majukumu mwamuzi wa ziada na kama mwamuzi wa katikati hafiki katika maeneo hayo anakuwa hajafika kwenye ubora anaotakiwa kufikiwa katika kuchezesha.