Timu ya Taifa ya Wanawake kuanza kambi
Timu ya Taifa ya Wanawake Twiga stars imeanza rasmi kambi yake tarehe 17 May,2021 kwenye makao makuu ya Shirikisho la Mpira wa miguu Tanzani kwa lengo la kuanza kujinoa kuelekea mashindano ya kufuzu AFCON.
Kambi hiyo inayotarajiwa kufanyika kwa takribani muda wa wiki tatu huku ikiwa inajumuisha jumla ya wachezaji 27 walioitwa kambini katika timu hiyo ili kuendelea kujifua na mazoezi baada ya kukatisha kambi yao ya mwisho baada ya Taifa kupata msiba wa aliyekuwa Raisi wa awamu ya tano hayati John Joseph Pombe Magufuli.
Na sasa timu hiyo inaingia kambini huku tayari ratiba ya mashindano ya kufuzu AFCON kwa wanawake ikiwa imetoka ambapo timu ya Taifa ya Tanzania ikiwa imepangiwa kukutana na timu ya Namibia katika mchezo wao wa kwanza unao tarajiwa kupigwa tarehe 8 July,2021 na mchezo wa marudiano ukitarajiwa kupigwa rarehe 15 ya mwezi huo.
Kocha mkuu wa timu hiyo ya Taifa Bakari Shime amesema kuwa wameanza kambi na wanatarajia kuanza mazoezi yao tarehe 18 July,2021 kuendelea mpaka wakati wa mchezo,huku akisema kuwa kikosi kipo kwenye hali nzuri isipokuwa kazi yao kubwa ya kwanza ambayo wanatarajia kuifanya kwa wachezaji hao ni kuyatoa mawazo yao kwenye ligi ambayo pia imetamatika mnamo tarehe 16 May,2021 na kuwarudisha wachezaji katika Utaifa.
Aidha kocha amesema wanaingia kambini kwenye maandalizi ya mwisho pamoja na kuangalia waliyojifunza kipindi cha nyuma kama endapo wachezaji wameyafanyia kazi na kuwaweka tayari kwa ajili ya mashindano hayo yaliyo mbele yao.
Kocha amewataka wadau wa soka kujitokeza katika kuisapoti timu hiyo ya Taifa ikiwa ni moja ya kushirikiana na Shirikisho la Mpira wa Miguu lakini pia kujitokeza kwa wingi uwanjani kama endapo itaruhusiwa siku ambayo watacheza mchezo wao dhidi ya Namibia.