‘Kilimanjaro Warriors’ Macho CECAFA

Kocha Kim Poulsen ametangaza rasmi kikosi cha vijana wa timu ya Taifa wenye umri chini ya miaka 23 watakao weka kambi kwa ajili ya kujiandaa kwenda kushiriki mashindano ya CECAFA yatakayofanyika nchini Ethiopia.

Poulsen ametangaza kikosi hicho kinachojumuisha jumla ya wachezaji ishirini (20), siku ya Ijumaa ya Julai 16, alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari za michezo yalipo Makao Makuu ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) ambapo kocha huyo alisema kuwa wanatarajia kuanza kambi hiyo mapema Julai 19 mwaka huu.

Wachezaji waliokwenye kikosi ni; Metacha Mnata, Rajabu Athuman, Daniel Mgore, Meshack Abraham, Wilbol Maseke, Israel Mwenda, Erick Mwijage, Nickson Kibabage, Andrew Simchimba, Lusajo Mwaikenda, Abdul Suleiman, Pascal Msindo, Oscar Masai, Abdulrazack Hamza, Lucas Kikoti, Abdulmajid Mangalo na Joseph Mkele.

Kocha Poulsen amesema kuwa kanuni za mashindano zimeruhusu wachezaji 3 wenye umri zaidi ya miaka 23; ambapo kwa upande wa kikosi chake amewajumuisha Sospeter Israel, Reliant Lusajo na Yusuph Mhilu walio na umri zaidi ya miaka 23.

Kikosi hicho cha Kilimanjaro Warriors kinatarajia kucheza mchezo wake wa kwanza dhidi ya Congo tarehe 22 mwezi Julai, huku mchezo wake wa pili dhidi ya Uganda ukitarajiwa kupigwa Julai 25, mwaka huu.