Pazia la Ligi Kuu Bara Lafungwa Rasmi

Ligi kuu ya Vodacom Tanzania Bara (Vodacom Premier League) imefikia tamati ambapo michezo yote tisa imepigwa kwenye viwanja tofautitofauti nchini huku baadhi ya timu zikitoka na furaha kwa kusalia katika ligi hiyo wakati timu nne zikiiaga ligi na timu nyingine mbili zenyewe kuangukia kwenye mechi za mtoano.

Katika michezo yote iliyochezwa 18 Julai, 2021 macho na masikio ya wapenzi na mashabiki wa soka yalikuwa kwa timu zilizokuwa kwenye kinyang’anyiro cha kushuka daraja na kusalia kwenye ligi hiyo ambapo timu za JKT Tanzania, Gwambina FC, Ihefu FC na Mwadui zilikuwa kwenye mstari mwekundu zikihitaji kujikomboa suala ambalo halikuwezekana; huku Coastal Union na Mtibwa nao wakiwa kwenye mstari wa njano  mguu sawa kucheza michezo ya mtoano (Play Off).

Matokeo ya michezo hiyo ya mwisho yalikuwa ni; Simba alifanikiwa kuifunga Namungo jumla bao 4-0, Biashara United akafungwa na Mbeya City bao 4-0 kwa sifuri, Coastal Union akashinda 3-1 dhidi ya Kagera Sugar, JKT Tanzania akaibuka na ushindi wa bao 2-1 dhidi ya Mtibwa huku  Ruvu Shooting wao wakikubali kipigo cha bao 1 kwa sifuri, kutoka kwa Azam FC.

Mechi nyingine zilikuwa ni kati ya KMC ambayo iliibuka na ushindi wa bao1 dhidi ya Ihefu iliyoambulia sifuri; Polisi Tanzania yenyewe ikailaza Mwadui kwa bao moja kwa sifuri pia wakati Tanzania Prisons (wajelajela) wao wakitoshana nguvu na Gwambina FC kwa kufungana bao 1-1. Kwa upande wa mabingwa wa kihistoria Young Africans na wao pia walitoka suluhu tasa dhidi ya Dodoma Jiji, mchezo huo ukipigwa katika uwanja wa Jumhuri Jijini Dodoma.

Baada ya michezo hiyo yote ya kufunga pazia la ligi kuu Tanzania bara kukamilika katika viwanja mbalimbali nchini; kwenye uwanja wa Mkapa Dar es Salaam penyewe palifanyika zoezi maalum la kukabidhi kikombe kwa mabingwa wa Ligi Kuu Bara kwa mara ya nne mtawalia Simba SC, huku John Bocco naye akifanikiwa kuwa mfungaji Bora wa ligi kwa msimu wa 2020/2021.

Kwa matokeo hayo, timu ya JKT Tanzania, Gwambina FC, Ihefu FC na Mwadui zimeiaga rasmi ligi Kuu Bara huku Coastal Union na Mtibwa nao wakiwa kwenye mstari wa njano  mguu sawa tayari kucheza michezo ya mtoano (Play Off).

Kuelekea michezo hiyo ya mtoano, timu ya Mtibwa Sugar itakwenda kucheza na timu ya daraja la kwanza Pamba FC ya Mwanza wakati Coastal Union wao wakienda kupepetana na timu ya jeshi yaTransit Camp FC. Michezo hiyo inatarajiwa kuchezwa kati ya tarehe 21 na 24 Julai, 2021 ambapo timu za ligi kuu zote zitaanzia ugenini.