Rais Karia Afungua Rasmi Kozi ya Ukufunzi Ngazi ya CAF
Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania(TFF) Wallace Karia amefungua rasmi kozi ya ukufunzi ngazi ya CAF Septemba 07, 2021 inayofanyika katika Makao Makuu ya Shirikisho hilo yaliyopo Ilala jijini Dar es salaam, ikijumuisha washiriki wapatao 11 kutoka Mikoa mbalimbali ya Tanzania Bara na Visiwani.
Kozi hiyo ya siku 10 ina lengo la kuzidi kuwajengea uwezo waalimu hao wa Mpira wa miguu ili waweze kufanya kazi yao kwa umakini na ueledi, lakini pia kuongeza idadi ya wakufunzi wa ndani ambao watakuwa na sifa za kufundisha mpira wa miguu kwa viwango vinavokubalika kimataifa.
Akizungumza wakati wa ufunguzi wa kozi hiyo Rais Karia alisema, anafurahishwa kuona jinsi waalimu walivokuwa na hamasa kubwa ya kupenda kujifunza vitu vipya katika mchezo wa mpira; kwani tasnia hiyo imendelea kukua na mambo mengi yanaongezeka kila kukicha hivyo kuongeza ujuzi ni jambo la lazima kwa waalimu wa mpira ili waweze kuendana na kasi ya mabadiliko hayo.
Akiongea kwa msisitizo Karia alitoa rai kwa wakufunzi wa kike kuendelea kujitokeza kwa wingi na kuchangamkia fursa pindi kozi hizi zinapotangazwa ili pawepo na usawa wa kijinsia katika tasnia hiyo na siyo kuwaachia wanaume peke yao .
Mbali na hayo aliongeza kwamba katika kipindi cha uongozi wake kozi hizi zitakuwa na mwendelezo na atahakikisha zinatolewa mara kwa mara katika ngazi zote akianza na ngazi ya mikoa huku akitolea mfano wa kozi za Grass roots zinazoendelea kutolewa na kusema kwamba kwa siku za usoni kozi hiyo itatolewa visiwani Zanzibar.
Naye Mkurugenzi wa ufundi Oscar Mirambo alisema kozi hiyo italeta matokeo chanya si tu kwa Tanzania bali Afrika kwa ujumla; kwani washiriki hao watakwenda kutatua changamoto mbalimbali zilizopo kwa waalimu wa mpira na kutengeneza wachezaji walio bora ambao watakuwa na uwezo wa kufanya vizuri katika mashindano yote watakayoshiriki.
Kwa upande wa mkufuzi wa kozi hiyo mwalimu Honor Janza ( Elite CAF Instuctor) yeye alisema anashukuru kwa mapokezi mazuri aliyoyapata kutoka kwa uongozi wa TFF lakini pia kwa shirikisho la mpira wa miguu barani Africa (CAF) kwa kumwamini kufundisha walimu wa mpira wa miguu nchini Tanzania hivyo atatoa elimu stahiki anayoamini kwamba itazalisha makocha wengi wenye ujuzi sahihi na watakaosimamia misingi ya kada yao vile inavyotakiwa ili hapo baadaye Tanzania iweze kuzalisha timu bora na waalimu wenye viwango bora watakaoweza kujiendesha bila kutengemea waalimu kutoka nje.
Kozi hiyo ya ukufunzi ngazi ya CAF ni mara ya kwanza kutolewa hapa nchini Tanzania Ikiwa ni moja ya mpango wa idara ya ufundi kupitia kitengo cha elimu (coach education) kuendelea kuwajengea uwezo wakufunzi wa ndani ili kuleta mabaliko chanya katika mchezo wa mpira wa miguu.