Ligi Yarejea na Utamu Wake, Waliopanda Waonja Chungu Tamu ya Ligi Kuu Bara

Namungo FC, Mbeya Kwanza, Dodoma Jiji na Mbeya City zimefanikiwa kuianza vyema Ligi Kuu Tanzania kwa kuanza na ushindi, huku Simba wao wakishindwa kutamba ugenini kwa Biashara United  huko Mkoani Mara katika muendelezo wa michezo ya Ligi hiyo ambapo leo  Septemba 28, 2021 michezo mitatu ilipigwa katika viwanja tofauti tofauti huku matokeo ya moja moja na suluhu yakitawala.

Mchezo wa mapema ulikuwa ni kati ya Dodoma Jiji na Ruvu Shooting; mchezo huo ukipigwa saa nane mchana (8:00) kwenye uwanja wa Jamhuri Jijini Dodoma, ambapo timu ya Dodoma Jiji ilifanikiwa kuibuka na ushindi wa bao 1-0 kabla ya Mbeya City nao kuwafunga watani wao Tanzania Prisons kwa goli moja kwa sifuri pia wakati huo huo Simba SC wao wakikwaa kisiki kwa wenyeji Biashara United waliogoma kuachia alama tatu kwenye ardhi ya nyumbani baada ya kutoka suluhu tasa.

Mnyukano ulikuwa makali katika michezo hiyo yote iliyopigwa katika madimba tofauti tofauti; kuanzia siku ya kwanza; kwani timu zote hazikufanikiwa kupata ushindi kirahisi, jambo linaloashiria ugumu wa Ligi ya msimu wa 2021/2022.

Halikadhalika michezo iliyopigwa Septemba 27 mwezi huu, ambapo  timu ya Mbeya Kwanza ilifanikiwa kuilaza Mtibwa Sugar kwa bao moja kwa sifuri; Namungo FC ikachalaza bakora mbili kwa nunge timu ya Geita Gold huku Azam FC nayo ikishikiliwa shati na Coastal Union katika mchezo uliopigwa kwenye uwanja wa Mkwakwani Jijini Tanga.

Kwa matokeo hayo hadi sasa timu ya Namungo ndiyo inashikiria uskani kwa kuwa na alama tatu na magoli mawili; ikifuatiwa na Dodoma Jiji, Mbeya City, na Mbeya Kwanza wenye goli moja na alama tatu.  Azam FC na Coastal Union wanawafukuzia kwa nyuma baada ya kuvuna alama moja moja  na goli 1-1  huku Biashara wakifuata kwa herufi na Simba akionekana kuwa nyuma yake.

Michezo mingine itaendelea Septemba 29, 2021 katika viwanja mbali mbali ambapo mechi kubwa na yenye kusubiriwa kwa hamu na wadau wengi wa soka ikiwa ni ile ya Mabingwa Kihistoria Young Africans dhidi ya wenyeji wao Kagera Sugar; mchezo utakaopigwa majira ya saa kumi jioni kwenye uwanja wa Kaitaba Mkoani Kagera.