Twiga Stars “COSAFA Muhimu Kwetu”

Timu ya Taifa ya ‘Twiga Stras’ ambayo ipo nchini Afrika Kusini kwa ajili ya mashindano ya ‘COSAFA Women’s Championship’ imeendelea na mazoezi ya kujiweka sawa tayari kuvaana na Zimbabwe kwenye mchezo wake wa kwanza unaotarajiwa kupigwa Septemba 29, 2021.

Kauli hiyo ilitolewa Septemba 28, 2021 na benchi la ufundi la timu linaloongozwa na Kocha Mkuu Bakari Shime walipokuwa wanaelekea kwenye mazoezi ya mwisho mwisho waliyokuwa wakifanya kwa ajili ya kujiimarisha zaidi kuelekea mchezo huo dhidi ya Zimbabwe.

Kocha Shime ambaye alijiunga na timu hiyo mapema asubuhi  ya Septemba 28, akitokea nchini Eritrea ambako alikuwenda na timu ya Taifa ya Wanawake U20 (Tanzanite) kwenye mchezo wa Kufuzu Kombe la Dunia ambapo kikosi hicho cha U20 kilifanikiwa kuibuka na ushindi wa bao 3-0 dhidi ya Eritrea. Kocha huyo aliambatana na baadhi ya wachezaji waliokuwa  huko kutimiza majukumu mengine kwenye timu ya U20. Miongoni mwa wachezaji hao ni pamoja na; Aisha Masaka (mfungaji wa magoli2) ,Clara Luvanga (mfungaji wa goli 1) na Enekia Kasongo.

Shime alieleza kuwa maandalizi yao yako vizuri na kwamba wachezaji wote wako tayari kwa mchezo wao wa awali lakini pia kuhakikisha wana shinda michezo yote na hatimaye kuondoka na kikombe hicho cha COSAFA Women’s Championship. Malengo yao makubwa  waliyojiwekea kama timu na Taifa kwa ujumla ni kuhakikisha wanatwaa ubingwa huo. Shime alieleza hayo mapema alipowasili nchini humo kabla hata ya kwenda kufanya mazoezi ya mwisho.

Aidha, alieleza zaidi juu ya malengo ya timu yake pamoja na TFF kuwa ni kwenda kushiriki mashindano ya Kufuzu AFCON tena kwa mafanikio makubwa. Hivyo, wanaamini ili kufikia malengo yao ni muhimu kwa wao kujiweka sawa kupitia mechi tofauti tofauti kwenye kila mashindano wanayoshiriki.

Mchezo wa kwanza wa ‘Twiga Stars’ dhidi ya Zimbabwe utapigwa kwenye uwanja wa Nelson Mandela Bay (NMB) mnamo majira ya saa 9:30 Alasiri kwa saa za Afrika Kusini , sawa na saa 10:30 kwa  saa za Afrika Mashariki .

‘Twiga Stars’ ambayo iliwasili Afrika Kusini Septemba27 2021, inajumla ya wachezaji 22 na ilifanya mazoezi yake ya mwisho kwenye uwanja wa Hearts katika mji wa Port Elizabeth uliopo pembezoni kidogo mwa Bahari ambako ndiko mashindano hayo ya COSAFA yatakakofanyikia ambapo michezo yote itapigwa ndani ya mji huo uliopo kwenye jimbo la Rasi ya Mashariki (Afrika Kusini).

Kikosi cha Twiga Stars kilichopo Afrika Kusini kwenye mashindano ya COSAFA Women’s Championship ni; Janeth Shija Simba, Anastazia Antony Katunzi, Eva Wailes Jackson, Amina Alli Bilali, Fatuma Issa Maonyo, Donisia Daniel Minja, Mwanahamisi Omary Shurua (Gaucho), Stumai Abdallah Athumani na Mwamvua Seif Haruna.

Wachezaji wengine ni;  Aisha Khamis Masaka, Diana Lucas Msewa, Janeth Christopher Pangawene, Koku Ally Kipanga, Clara Cleitus Luvanga, Julitha Aminiel Tamuwai Singano, Zawadi Hamisi Athumani, Enekia Kasonga Lunyamila, Opa Clement Tukumbuke Sanga, Happiness Hensron Mwaipaja, Zubeda Mohamed Mgunda, Husna Zuberi Mtunda na Mariam Yusuf Juma.

Timu ya ‘Twiga Stars’ ya Tanzania ipo kwenye kundi ‘B’ pamoja na Zimbabwe atakaye shuka naye dimbani kwenye mchezo wa kwanza, Botswana atakaye kutana naye kwenye mchezo wa pili na  Sudani Kusini ambayo watavaana kwenye mchezo wa mwisho utakao amua nani anatupwa nje na nani ataendelea mbele kwenye safari hiyo ya COSAFA Women’s Championship 2021.