Balozi Awataka Twiga Stars Kufika Fainali COSAFA

Timu ya Taifa ya Tanzania Twiga Stars imetakiwa kufika hatua ya fainali ili kuleta hamasa kwa watanzania wote, lakini pia iwe pongenzi kwa Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuwa Rais wa kwanza mwanamke kutoka Tanzania na kuhutubia kwenye Mkutano wa Baraza Kuu la umoja wa Mataifa halikadhilika kuwapa furaha wananchi waishio nchini Afrika ya Kusini pamoja na kuzidi kuitangaza Tanzania Afrika na Duniani kote.

Akizungumza na timu ya Twiga Stars na uongozi mzima uliambatana kwenda kwenye mashindano ya COSAFA nchini Africaka Kusini mwishoni mwa mwezi Septemba, 2021 Mhe. Balozi wa Tanzania nchini Afrika Kusini Meja Generali Gaudence Milanzi ameahidi kufika kujumuika na watanzania wenzake ili kutoa sapoti kwa timu yake ya Tanzania kwa kwenda kuushuhudia mchezo huo mubashara kabisa Uwanjani hapo siku hiyo ya mchezo huo.

Mheshimiwa Balozi aliyasema hayo alipowaalika wachezaji wa timu hiyo Pamoja na viongozi walioambatana nao kupata kwa Pamoja chakula cha mchana ambapo alisema kuwa yeye Pamoja na timu yake ipo tayari kufunga safari kutokea mjini Johannesburg mpaka Port Elizabeth kwenda kushuhudia mchezo wa Fainali endapo tu timu hiyo itafikia hatua hiyo.

Twiga Stars ambao tayari wamekwisha wasili Port Elizabeth nchini Afrika Kusini asubuhi ya Septemba 27, 2021 na kupata mwaliko wa kula chakula cha mchana Pamoja na Balozi Septemba 26 mara baada ya kufika mjini Johannesburg kabla ya kuanza safari ya takribani masaa 13 kuelekea Port Elizabeth ambako ndiko mashindano hayo yatafanyika.

Timu ilipokelewa na maafisa wengine kutokea Ubalozini na kuongoza msafara huo kuelekea kwenye Hotel ya Garden Court ambako  walipata fursa ya kukutana na mwenyeji wao Balozi Meja Generali Gaudence Milanzi.

Mhe. Balozi alisema kuwa Jumuiya ya Watanzania waliopo nchini Afrika Kusini imefurahi sana ujio wa timu ya Twiga na hasa lengo lao lilikuwa ni kufika wote kuipokea timu hiyo isipokuwa kutokana na ugonjwa wa UVIKO 19 ndiyo wakaonelea kuwakilishwa na Mwenyekiti wa Jumuiya hiyo Alex Minja.

Eiza alieleza kuwa ni heshima kubwa ambayo timu ya Twiga Strasr imekuwa ikiipatia nchi ya Tanzania kwa kufanya vizuri kwenye mashindano mengi ambayo imekuwa ikishiriki na kwamba anaamini hiyo yote ni kutokana na moyo wa kupenda na kutumikia nchi kwa wachezaji ndio chachu kubwa anayoiona kwa timu hiyo.

Viongozi wengine waliokuwepo ni Katibu Mkuu wa TFF Kidao Willfred aliyekuwa na msafara wa timu, Mwenyekiti wa Jumuiya ya Tanzania Alex Minja, Mwambata fedha wa Ubalozi Nyalwera Rweyemamu na Bi Aisha ambaye alikuwa akishughulikia taratibu zote za kuhakikisha jinsi timu ya Twiga itakavyo fanya shughuli zake kwa kipindi chote nchini Afrika Kusini.