Timu ya Taifa ya Tanzania ya Wanawake “Twiga Stars” imekuwa timu ya kwanza kufuzu nusu fainali ya mashindano ya Cosafa kwa Wanawake baada ya kuibuka na ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Botswana.

Ushindi huo unamaanisha hakuna timu itakayoweza kuizidi katika Kundi B hata kama Botswana na Zimbabwe wanaoweza kufikisha alama 6 wakishinda katika michezo yao iliyosalia kutokana na kanuni za mashindano.

Kanuni za mashindano hayo inaanza kutazama michezo ambayo timu hizo zimekutana kama zitalingana alama, hiyo inatoa nafasi kwa Tanzania ambayo imezifunga timu hizo na tayari ikiwa imefikisha alama 6.

Mabao ya Twiga Stars katika mchezo huo dhidi ya Botswana yalipatikana katika kila kipindi yakifungwa na Donisia Minja na Mwanahamisi Omary.

Twiga Stars imesaliwa na mchezo mmoja dhidi ya Sudan Kusini ukiwa ni mchezo wa kukamilisha ratiba baada ya kuikata tiketi ya kucheza nusu fainali.