Twiga Stars Uso kwa Uso na Zambia Nusu Fainali
Timu ya Taifa ya Tanzania Twiga Stars inayoshiriki mashindano ya COSAFA Women’s Championship 2021 yanayofanyika Port Elizabeth nchini Afrika Kusini inatarajia kushuka dimbani kucheza mchezo wake wa nusu fainali dhidi ya timu ya Taifa ya Zambia Oktoba 07, kwenye dimba la Nelson Mandela Bay mnamo majira ya saa 12:00 mchana kwa saa za Afrika Kusini.
Twiga Stars ndio timu ya kwanza kwenye mashindano hayo kuweza kufuzu hatua ya nusu fainali mara baada ya kumpiga Botswana mabao 2-0 katika mchezo wao wa pili hatua ya makundi, mchezo uliochezwa Oktoba 02, 2021 kwenye uwanja wa Madibaz.
Kufuatia matokeo hayo timu ya Taifa ya Tanzania (Twiga Stars) ilijihakikishia kutofikiwa na yeyote kwenye kundi ‘B’ kwa kufikisha jumla ya alama sita licha ya kuwa kila mmoja katika kundi hilo kubakiza mchezo mmoja wa mwisho kukamilisha hatua ya makundi.
Ushindi huo dhidi ya Botswana, uliifanya Twiga Stars kuanza kujiweka sawa kuelekea hatua ya nusu fainali sambamba na maandalizi ya kukamilisha mchezo wake wa mwisho kwenye hatua ya makundi ambao ulichezwa Oktoba 04, 2021 na kutoka kifua mbele kw mabao 3-0 dhidi ya Sudani Kusini.
Stars ndiyo timu ilioweka rekodi ya kutangulia hatua ya nusu fainali, COSAFA Women’s Championship 2021 huku ikiwa pia ndio timu pekee kwenye kundi ‘B’ ambayo haikupoteza mchezo wake wowote wala kuruhusu goli lolote kwenye hatua hiyo ya makund.
Twiga Stars anakwenda kukutana na timu ya Taifa ya Zambia kwenye hatua ya nusu fainali, huku kila mmoja akiwa na jumla ya alama 09 nafasi ya kwanza kwenya kundi lake.
Kocha Mkuu wa Twiga Stars Bakari Shime alisema anashukuru Mungu kwa timu yake kuweza kufuzu katika hatua hiyo na kwamba wamejiandaa vizuri kwa mchezo licha ya timu ya Zambia kuonekana kuwa bora kutokana na rekodi sawa ambazo Twiga Stars na Zambia wanazo katika mashindano hayo 2021.
Hata hivyo, alisema anatarajia mchezo huo kuwa mgumu kutokana na ubora ambao wote wanao na kwamba anaamini kuwa ubora wa timu mara zote unafahamika baada ya kupambana na mpinzani aliye bora pia.
Kwa upande wake Katibu Mkuu wa TFF Kidao Wilfred alisema kuwa hatua hiyo iliyowezwa kupigwa na Twiga Stars kwenye mashindano hayo, kwao wao kama Shirikisho ni mafanikio makubwa kwani ndiyo matarajio ambayo TFF imejiwekea katika mpira wa Miguu kwa Wanawake.
Kidao Wilfred aliongeza kuwa kwa uongozi uliopo madarakani tangu 2017 chini ya Rais Wallace Karia moja ya vipaumbele vyake ni kuhakikisha soka la wanawake linazidi kupiga hatua kwa kuhakikisha TFF inasimamia kila hatua katika kukuza mpira huo kwa Wanawake.
Aidha, Kidao alisema kuwa kwa TFF timu ya Taifa kupata nafasi ya kushiriki mashindano makubwa kama hayo tayari ni mafanikio makubwa kwani anaamini hiyo ndiyo njia sahihi ya wao kuweza kufahamu mni kwa kiasi gani wameweza kufikia matarajio ya mipango mkakati waliojiwekea kwenye uongozi wao.
Katibu Mkuu wa TFF pia amefurahishwa sana kwa hatua ambayo Twiga Stars wameweza kupiga kwenye mashindano hayo sambamba na kuweka rekodi ya kuchukua tuzo za wachezaji bora katika kila mchezo waliocheza kwenye hatua ya makundi.
Mechi mbili za nusu Fainali zitapigwa Oktoba 07, 2021ambapo Twiga Stars atashuka DIMBANI kukupiga dhidi ya timu ya Zambia kwenye uwanja wa Nelson Mandela Bay majira ya saa 12:00 mchana, na mchezo mwingine utawakutanisha timu ya Taifa ya Afrika Kusini na Malawi majira ya 9:30 mchana kwenye uwanja wa Nelson Mandela Bay.
Matokeo ya nusu fainali hizo mbili ndizo zitakazo toa taswira halisi kuwa nani anakwenda kucheza fainali na timu zipi zitakazo kwenda kuvaana kwa ajili ya kutafuta mshindi wa tatu.