Twiga Stars Kukutana na Malawi Fainali

Timu ya Taifa ya Tanzania Twiga Stars inayoshiriki mashindano ya COSAFA Women’s Championship 2021 yanayoendelea nchini Afrika Kusini inatarajia kushuka dimbani kuminyana na timu ya Taifa ya Malawi kwenye mchezo wa Fainali unaotarajiwa kupigwa Oktoba09, 2021 kwenye dimba la Nelson Mandela Bay majira ya saa 9:00 alasiri

Twiga Stars imeweza kufuzu kwenye hatua hiyo ya Fainali mara baada ya kupata ushindi kwenye mchezo wake wa nusu fainali uliochezwa dakika tisini pasipo mshindi na hatimaye kwenda kwenye mikwaju ya penati ambapo timu hiyo ya Twiga Stars iliweza kuibuka kidedea dhidi ya timu ya Taifa ya Zambia; mchezo huo ukichezwa katika uwanja wa Nelson Mandela Bay mnamo majira ya saa 6:00 mchana kwa saa za Afrika Kusini sawa na saa 7:00 mchana kwa saa za Afrika Mashariki.

Mchezo huo uliobidi kwenda kwenye hatua ya kupiga mikwaju ya penati haukuwa rahisi kwa timu zote mbili na kupelekea  dakika 90 za mchezo huo kutamatika kwa matokeo ya kufungana bao 1-1 baada ya Zambia kusawazisha bao Mnamo dakika ya 69 lililofungwa na Grace Chanda (JZ 10).

Kabla ya matokeo hayo timu ya Twiga Stars ilikuwa mbele kwa bao moja ambalo lilipatikana kwa timu ya Zambia kujifunga katika kipindi cha kwanza (dk45), kwa matokeo hayo ambayo yalidumu mpaka kipyenga cha mwisho cha mwamuzi kinapulizwa ndiyo yaliyopzipeleka timu hizo kwenye hatua ya kupiga mikwaju ya penati.

Mikwaju ya Penati ndiyo iliyo wapatia ushindi Twiga Stars mara baada ya kupachika nyavuni mipira mitatu na kupoteza moja kati ya penati nne walizo piga, huku kwa upande wa Zambia wenyewe wakipachika mipira miwili pekee kati ya penati  nne walizo piga.

Wafungaji wa magoli ya Penati ni ; Fatuma Suleiman (Densa JZ 05), Opa Tukumbuke Clement (JZ 18) na Enekia Kasonga (JZ 17). Kwa matokeo hayo sasa ni faida kwa Twiga Stars ambaye anakwenda kwenye hatua ya Fainali ambapo huko anatarajia kushuka dimbani na Malawi ambao nao wameshinda kwenye mchezo wao wa nusu fainali dhidi ya Afrika Kusini kwa ushindi wa mabao 3 – 2.

Mkuu wa Twiga Stars Bakari Shime alikipongeza kikosi chake kwa kufanya vizuri licha ya kuwakosa baadhi ya wachezaji  kwenye mchezo huo hata hivyo alisema kwa makosa madogo madogo yaliyoweza kujitokeza watakwenda kuyafanyia kazi kabla ya kushuka dimbani kwenye mchezo wa Fainali. Kocha Shime alisema kuwa licha ya mchezo huo kuwa mgumu bado anaamini maandalizi yao ndiyo yaliyopelekea wao kupata matokeo hayo ya ushindi.

Timu ya Taifa ya Twiga Stars imeendelea pia kuchukua tuzo za mchezaji bora kama ambavyo wanafanya katika kila mchezo kwenye mashindano hayo, ikumbukwe kuwa Twiga Stars imecheza michezo mitatu kwenye hatua ya makundi na katika michezo yote hiyo imekuwa ikichuka tuzo ya mchezaji bora katika kila mchezo.

Mchezaji bora katika mchezo wa kwanza alikuwa ni Mwanahamisi Omary, mchezo wa pili; Fatuma Suleiman, mchezo wa tatu; Stumai Athumani na mchezo wanne ambao ni wa nusu fainali amechukua tuzo hiyo nahodah wa kikosi hicho Amina Ally Bilali.

Mashindano ya COSAFA Women’s Championship (2021) yatamalizika Oktoba 09, 2021 kwa kupigwa mchezo wa fainali kati ya Twiga Stars na Malawi katika dimba la Nelson Mandela Bay; mchezo huo ikitarajiwa kuchezwa mnamo  majira ya saa 9:00 alasiri wa saa za Afrika Kusini sawa na saa 10:00 jioni kwa saa za Afrika Mashariki. Mara baada ya kumalizika kwa mchezo  wa kumtafuta mshindi wa tatu kati ya Afrika Kusini na Zambia ambao utachezwa majira ya saa 6:00 mchana Afrika Kusini sawa na saa 7:00 mchana kwa saa za Afrika Mashariki.