Tanzanite Queens Kuivaa Eritrea Chamazi

Kikosi cha timu ya Taifa ya wanawake wenye umri chini ya miaka 20 Tanzania (Tanzanite Queens) kinatarajia kushuka dimbani hapo kesho 09 /1O/2021 katika mchezo wa marudiano dhidi ya timu ya Eritrea katika Dimba la Azam Complex, Chamazi Jijini Dar-es Salaam, ikiwa ni katika harakati za kuisaka tiketi ya kufuzu kushiriki Kombe la Dunia huko nchini Costa Rica 2022.

Akizungumza na waandishi wa habari kuelekea katika mchezo huo Kocha Msaidizi wa kikosi hicho Edna Lema alisema, kikosi chake kimejiandaa vizuri na kimefanya mazoezi ya kutosha ambayo yatawahakikishia kupata ushindi mnono zaidi ya ule walioupata katika mchezo wa ugenini nchini Eritrea.

Edna aliendelea kusitiza kwamba licha ya kupata ushindi mnono ugenini haimaanishi kwamba makosa hayakufanyika, hivyo wametambua makosa yao na wamejitahidi kurekebisha kwa kiasi kikubwa wakati wote waliokuwa mazoezini. Kocha Edna anaamini wachezaji watazingatia maelekezo hayo na kuyatumia ipasavyo wakati wa mchezo huo na hatimaye kuweza kupata matokeo mazuri ambayo yatazidi kuipeperusha vyema Bendera ya Tanzania katika anga za Kimataifa.

Kwa upande wa kocha msaidizi wa kikosi cha Timu ya Taifa ya Eritrea Demsas Tekeste, alianza kwa kuushukuru uongozi wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) kwa kuwakarimu vizuri tangu walipofika Tanzania huku akisema hajapata changamoto yoyote mpaka hivi sasa kuelekea katika mchezo wa marudiano dhidi ya Tanzania. Kocha huyo alisema wamejiandaa vizuri kwa mchezo licha ya kwamba kikosi chake kuwa na majeruhi wapatao watatu lakini bado  haitawazuia wao kupata ushindi.

Naye nahodha wa Tanzanite Queens Irene Elias Kisisa alisema kikosi kiko tayari kwa mchezo na wachezaji wote wana ari kubwa na mchezo hivyo akawatoa hofu watanzania kwa kuwaahidi kuwa Tanzanite kushiriki World Cup 2022 ni lazima. Irene alisema kuwa wao wamejipanga kushinda kila mechi na wanachukulia kila mechi mbele yao kuwa ni fainali.

Rahwa Tewolde ambaye ni nahodha wa Eritrea alisema wanaingia katika mchezo wa marudiano wakiwa na kumbukumbu ya kupoteza nyumbani hivyo mchezo huu utawapa nafasi wao kubadilisha kumbukumbu hiyo na kuweza kushinda huku akisisitiza kwamba tumekuja kushinda na tutashinda.

Tanzanite Queens watashuka Dimbani wakiwa na mtaji wa goli 3 magoli yaliyofungwa katika mchezo wa awali uliochezwa kunako Dimba la Asmara, nchini Elitrea, wafungaji wa magoli hayo wakiwa ni Aisha Masaka pamoja na Clara Luvanga.