Young Africans Kiungo Kimekolea, Yatoa Dozi Nyingine kwa Azam  FC 

Mchezo uliowakutanaisha Young Africans dhidi ya Azam FC ulimalizika kwa timu ya Young Africans kuichabanga Azam kwa mabao mawili kwa sifuri.

Mchezo huo uliopigwa Oktoba 30, 2021 majira saa 1:00 usiku kwenye uwanja wa Mkapa ulikuwa na mvuto wa aina yake huku timu ya Young Africans ikifanikiwa kuutawala mchezo huo katika vipindi vyote na kuwafanya Azam FC kushindwa kuambulia hata bao la kufutia machozi.

Timu zote ziliuanza mchezo huo taratibu katika dakika za awali, huku kila timu ikiwa makini ili kutoruhusu bao la mapema ambalo lingeweza kuinyong’onyeza na kusababisha kupoteza mchezo huo kwa idadi kubwa ya mabao, jambo ambalo kila timu haikutaka litokee.

Kabumbu liliendelea kutandazwa dimbani hapo huku timu zote zikijaribu kutengeneza nafasi za magoli; Young Africans wao walikuwa wa moto zaidi ambapo walifanikiwa kutengeneza mashambulizi mengi ambayo yalipekea wao kuandika bao la kuongoza kunako dakika ya 37 kipindi cha kwanza kupitia kwa Fiston Mayele(9) na kuzifanya timu hizo kwenda katika mapumziko kwa tofauti ya bao moja kwa sifuri.

Kipindi cha pili Young Africans walirejea wakiwa na moto zaidi ambapo walizidisha mashambulizi huku wakiupiga mwingi na kufanikiwa kuandika bao la pili kwenye dakika ya 73; bao hilo likifungwa na Jesus Moloko (12). Hata hivyo, si haba Azam nao walionesha kuwa wapo uwanjani kwa kufanya kosakosa kadhaa japokuwa hazikuweza kuzaa bao lolote mpaka dakika 90 za mchezo huo zinatamatika.

Kocha wa Young Africans Nasreddine Nabi Mohammed baada ya mchezo huo alisema kuwa timu yake ilijiandaa vizuri kwa kuwa alijua kabisa ubora na ukubwa wa Azam. Alieleza kwamba timu yake ilicheza vizuri na ilifanikiwa kutengeneza nafasi za kutosha licha ya kushindwa kuzitumia ipaswavyo bado ushindi walioupata unatokana na kiwango kizuri walichokionesha katika mchezo huo.

Nabi aliongeza kuwa timu yake bado inahitaji muda zaidi ili iweze kufikia kiwango ambacho wanayanga wanakitaraji hivyo bado yeye pamoja na benchi la ufundi wanaendelea kukiandaa kikosi hicho ili kiweze kuwa cha kimataifa zaidi na kiweze ogopeka Afrika sio kwenye ligi ya Tanzania ya NBC pekee; kwani mpaka hapo kilipofikia kikosi chake ni asilimia 47-50 tu ya matarajio yake na kwamba bado anahitaji muda zaidi ili kiweze fikia asilimia 90 hadi 100.

Aidha, kocha huyo alikisifu kikosi cha Azam FC na kusema kuwa kimejitahidi kuizua safu ya ushambuliaji ya Young Afrika isiweze kuleta madhara makubwa, hivyo alimsifu kocha George Lwandamina kwa kuonesha upinzani mkubwa licha ya kupoteza mchezo huo kwani anaamini kuwa Azam ni timu yenye uwezo mkubwa.

Kwa upande wake kocha msaidizi wa Azam FC Vivier Bahati yeye alisema kuwa timu yake ilicheza vyema japokuwa haikuweza kupata matokeo mazuri katika mchezo huo kutokana na ubora wa wapinzani wao. Alidai pia, kukosekana kwa umakini wa kutosha kwa kikosi hicho ndiko kulipelekea kuadhibiwa kutokana na makosa kilichoyafanya katika nyakati tofauti tofauti na kwa sababu Young Africans walikuwa vizuri zaidi walifanikiwa kuyatumia makosa waliyoyafanya na kujipatia mabao.

Kocha huyo alibainisha ya kwamba kupoteza kwa mchezo huo kulitokana pia na kuzidiwa katika baadhi ya maeneo hasa ya katikati ambapo Young Africans wao walifanikiwa kumiliki sehemu ya kiungo, huku safu ya ulinzi na ushambuliaji ikiwa kwenye ubora wa hali ya juu.  Bahati alitaja kuwa mlinda mlango wa Young Africans naye alikuwa kikwazo kikubwa kwao. Pamoja na hayo, kocha Bahati alisema kuwa mchezo huo umepita na sasa wanajipanga kwa ajili ya michezo ijao, kwani ligi bado ndefu.

Naye Mkurugenzi wa Ufundi wa kikosi cha vijana wa Klabu ya Young Africans Mwinyi Zahera alisema kuwa timu yao bado haijapata muunganiko mzuri licha ya kupata matokeo mazuri na kwamba wanahitaji kucheza mechi sita zaidi ili kuweza kukaa sawa. Zahera alidai kuwa Young Africans wanakikosi kilichosheheni wachezaji bora wanaocheza kwenye timu zao za taifa huku akieleza ubora wa golikipa wa timu hiyo Djigui Diarra ambaye amekuwa bora zaidi katika kuipanga timu pindi wawapo uwanjani.

Katika mchezo mwingine uliopigwa mapema majira ya 10:00 jioni kwenye uwanja wa Uhuru, timu ya Dodoma Jiji ilifanikiwa kuichapa Mtibwa Sugar kwa bao 1-0; bao lililofungwa dakika ya 48 kipindi cha pili baada ya dakika 45 za kipindi cha kwanza kutamatika pasipo kufungana. Katika michezo iliyopigwa Oktoba 29 ikizikutanisha Mbeya Kwanza na Biashara United ambapo timu hizo ziliktoka sare ya 1-1 huku KMC wao wakipokea kipigo cha bao moja kutoka kwa Kagera Sugar wakiwa aridhi ya nyumbani.

Kwa matokeo hayo Young Africans anaendelea kusalia kileleni mwa ligi akiwa na alama (12), akifuatiwa na Dodoma Jiji (10), Polisi Tanzania nafasi ya tatu (9), Kagera Sugar akiwa nafasi ya nne (8) huku Simba akiwa katika nafasi ya tano na alama (7) kabla ya mchezo wake wa Oktoba 31, 2021 dhidi ya Coastal Union ya Tanga.