TFF yawapiga msasa waamuzi.

Shirikisho la mpira wa miguu Tanzania (TFF) linaendesha semina ya siku tatu kwa waamuzi wa ligi kuu Tanzania Bara (NBC Premier League) pamoja na kamati ya waamuzi kuanzia leo februari 15, 2022 kwenye uwanja wa Benjamin Mkapa ili kutazama na kupitia changamoto zilizojitokeza katika mzunguko wa kwanza wa ligi kwa lengo la kuboresha maeneo mbalimbali yaliyokuwa na mapungufu.

Akizungumza wakati wa ufunguzi wa semina hiyo Kaimu Katibu mtendaji wa Baraza la Michezo la Taifa (BMT) Bi. Neema Msitha ameipongeza TFF pamoja na TPLB kwa kuandaa semina hiyo kwani inatoa nafasi kwa waamuzi kujitathimini na kurekebisha makosa yaliyojitokeza katika ligi jambo ambalo litapelekea kuwa na ligi bora na yenye mvuto, pia aliwapongeza waamuzi kwa kufika kwa wingi katika semina na hii ikitoa taswira ya utayari walionao katika kujifunza na kuongeza ujuzi katika taaluma yao.

Kaimu Katibu huyo ametoa wito kwa waamuzi akiwataka kuilinda na kuitunza taaluma yao ili hadhi ya mchezo wa soka hususani soka la Tanzania izidi kupanda na kufikia katika viwango vya juu, huku akitilia mkazo wa umuhimu wa michezo kuwa ndio kitu pekee kinachowaunganisha watu pale ambapo vyombo vingine vimeshindwa.

Naye mwenyekiti wa kamati ya waamuzi Nassor Hamduni aliwataka waamuzi kuzingatia yote watakayofundishwa katika semina na kuhakikisha wanayafanyia kazi, lakini kubwa zaidi ni kuendelea kuzitafsri sheria 17 za soka pindi wanapokuwa uwanjani kwa ufasaha. Mwenyekiti huyo alisema anaamini baada ya semina hiyo matokeo chanya yataonekana toka kwa waamuzi hasa kwenye mzunguko wa pili wa ligi kuu Tanzania bara.

Semina hiyo ya waamuzi inatarajia kumalizika siku ya Alhamis ya Februari 17,2022 ikiwa ni utaratibu wa kawaida kwa TFF kwa kila nusu ya msimu wa ligi unapomalizika.