28 Waitwa Kambini Taifa Stars.

Kocha mkuu wa timu ya Taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’ Kim Poulsen leo ametangaza majina ya wachezaji 28 watakoingia kambini tayari kujiandaa kwa michezo miwili ya kirafiki ya kimataifa kwa mujibu wa kalenda ya FIFA, pamoja na kufanya maandalizi ya mwanzo kuelekea katika mashindano ya kufuzu AFCON pamoja na CHAN.

Akizungumza na waandishi wa habari katika makao makuu ya TFF Poulsen alisema michezo yote miwili itachezwa nyumbani katika dimba la Benjamini Mkapa. Mchezo wa kwanza utachezwa tarehe 23.03.2022 dhidi  ya Africa ya kati (Central Africa Republic) na baadaye tarehe 29.03.2022 watacheza dhidi ya Sudani na baada ya mchezo huo  kambi itavunjwa rasmi.

Poulsen aliendelea kusema kwamba timu zote mbili ambazo kikosi chake kitakutana nazo hazijapishana sana katika viwango vya FIFA (Central African Republic nafasi ya 114, Sudan 127), hivyo michezo hiyo ni muhimu sana kwa kikosi chake kwani itatoa taswira ya uwezo walionao wachezaji kuelekea katika michezo mingine ya kimataifa hususani AFCON itakayofanyika mwezi wa sita ambapo stars inatarajia kucheza michezo 4 ya kufuzu na baadaye mwezi Septemba watamalizia mechi 2.

Mbali na hayo Kim Poulsen alisema “michezo hii ya kalenda ya FIFA itatoa wasaa  kwa wachezaji chipukizi ambao hawajawahi kuwa sehemu ya kikosi cha stars lakini wameonyesha uwezo mkubwa katika klabu zao. Wakati sasa umefika kwa wachezaji chipukizi kupewa nafasi ili kuonyesha uwezo wao na kuliwakilisha taifa lao vizuri kwasababu hatuwezi kuwa na wachezaji wale wale kila siku”.

Wachezaji walioitwa kambini ni pamoja na Aishi Manula (Simba SC), Metacha Mnata (Polisi TZ), Abutwalib Mshery (Young Africans), Shomary Kapombe (Simba Sc) Israel Mwenda (Simba SC), Haji Mnoga (Weymouth-Uingereza), Dickson Job (Young Africans), Bakari Mwanyeto (Young Africans), Lusajo Mwamnyeto (Young Africans), Lusajo Mwaikenda (Azam Fc), Abdulrazak Hamza (Namungo Fc), Mohamed Hussein (Simba SC), Nickson Kibabaje (KMC), Farid Mussa (Young Africans).

Wengine ni Novatus Dismas (Beitar Tel Aviv Bat Yam –Israel), Mzamiru Yassin (Simba SC), Jonas Mkude (Simba SC), Zawadi Mauya (Young Africans), Aziz Andabwile (Mbeya City), Simon Msuva (Wydad-Morocco), Kelvin John (Genk-Belgium), Feisal Salum (Young Africans), Ben Starkie (Spalding- Uingereza), Mbwana Samatta (Antwerp-Ubelgiji), Tepsi Evance (Azam FC), Reliants Lusajo Namungo FC), Kibu Denis (Simba SC), George Mpole (Geita Gold) na Ibrahim Joshua (Tusker-Kenya).

Kikosi cha Taifa Stars kinatarajiwa kuingia kambini siku ya jumapili (20.03.2022) na watakaa kambini kwa muda wa siku 9.