Stars Yaichapa Afrika ya Kati kwa Mkapa
Timu ya taifa ya Tanzania “Taifa Stars” imefanikiwa kuilaza kwa jumla ya mabao 3 kwa 1 timu kutoka Jamhuri ya Afrika ya Kati katika Mchezo wa kirafiki wa Kimataifa uliopigwa Machi 23, 2022 kwenye uwanja wa Benjamin Mkapa na kuicha timu hiyo mdomo wazi.
Mchezo huo uliochezwa majira ya saa 1:40 ulianza taratibu huku timu zote zikishambuliana kwa zamu wakati kila timu ikichukua tahadhali kuruhusu bao la mapema. Hata hivyo, mnamo dakika ya tisa ya mchezo huo Stars ilifanya shambulizi kali la kushitukiza lililopelekea walinzi wa timu pinzani kufanya makosa na Tanzania kupata faida ya mpira wa kufa uliopigwa kiufundi na kiungo Novatus Dismas aliipatia timu yake bao la kuongoza lililodumu hadi timu hizo zinakwenda kwenye mapumziko.
Kiipindi cha pili timu zote zilifanya mabadiliko kwa kuwatoa wachezaji kadhaa ambayo yaliongeza nguvu kwa pande zote kwani kipindi ch apili, Stars ilifanikiwa kupata bao la pili kupitia mchezaji wa Kimataifa na nahodha wa kikosi cha Stars, Mbwana Samtta aliyepokea mpira kutoka kwa Farid Mussa na kuukwamisha kimiani kwa guu lake la kushoto.
Baada ya dakika chache wapinzani wa Stars walicharuka na kupeleka mashambilizi kwa kasi yaliyoilazimisha beki ya Stars kucheza madhambi kwenye eneo la hatari na hivyo kusabisha mkwaju wa penati iliyopachikwa kimiani na mchezaji aitwae Yawanendji Theodore jezi (18) na kuufanya ubao usomeke mbili kwa moja kabla George Mpole hajakomela msumari wa tatu na wa mwisho ulioifanya Stars kuibuka kidedea kwa jumla ya mabao 3-1.
Kocha wa Stars Kim Poulsen baada ya mchezo huo alisema kikosi chake kimecheza vizuri licha ya makosa ya hapa na pale ambayo yeye pamoja na benchi lake la ufundi wamekwishayabaini na kwamba wataendelea kuyafanyia kazi kadri iwezekanavyo ili kikosi kiweze kuwa imarika na kuwa bora zaidi.
Naye kocha wa timu ya Jumhuri ya Afrika ya Kati Savoy Raoul alisema kikosi chake kimeshindwa kufanya vizuri na kupoteza mchezo kutokana na sababu mbalimbali kubwa ikiwa ni baadhi ya wachezaji wake tegemeo kushindwa kucheza kufuatia changamoto zilizojitokeza kwa upande wake. Hata hivyo, bado anaimani na kikosi chake kuwa endapo kingekamilika huenda matokeo yasingeweza kuwa hayo.
Mchezo huo wa kirafiki wa kimataifa umechezwa kwa mujibu wa kalenda ya FIFA, Taifa Stars bado inatarajia kucheza michezo mingine miwili ya namna hiyo ili kufikisha michezo mitatu ikiwa ni sehemu ya maandalizi ya michuano ya kimataifa inayotarajiwa kuanza miezi ya hivi karibuni.