Serengeti Girls Kamili Kuikabiri Burundi

Timu ya Taifa ya wasichana chini ya umri wa miaka 17, Serengeti Girls inatarajia kuondoka hii leo kuelekea Ngozi nchini Burundi tayari kwaajili ya mchezo wake wa hatua ya pili ya Kufuzu Kombe la Dunia dhidi ya Burundi Aprili 16, 2022.

Serengeti Girls iliweka kambi Bukoba tangu mwanzoni mwa wezi Aprili na imemaliza mazoezi yake ya mwisho Aprili 13, 2022 ikiwa na jumla ya wachezaji 26 wote wakiwa tayari kwaajili ya mechi hiyo.

Akizungumza baada ya mazoezi yao ya mwisho waliyokuwa wakifanya kwenye uwanja wa Kaitaba kocha mkuu Bakari Shime alisema kuwa wamejiandaa vya kutosha na kwamba wanaimani timu yao itafanya vizuri  kwenye nyanja zote hususani kimbinu.

“Tunamshukuru Mungu leo tumevunja kambi ya kujiandaa na mchezo wetu dhidi ya Burundi, unaotarajiwa kuchezwa Aprili 16. Tumejiandaa kwaajili ya mechi hiyo ya ugenini na tunauzoefu wa aina hii ya mashindano.” Alisema Shime

Serengeti Girls imetinga hatua hiyo baada ya kuiondosha Botswana kwenye hatua ya awali kwa kuichapa kwa jumla ya mabao 11 katika mechi ya ugenini na nyumbani.