Serengeti Girls Yaendelea Kujifua Kuimaliza Burundi
Timu ya Taifa ya wasichana ya U17 ‘Serengeti Girls’ iliyondoka jana kwenda Visiwani Zanzibar imeendelea na mazoezi yake hii leo Aprili 20, 2022 ikiwa ni katika harakati za kujiandaa na mchezo wa marudiano dhidi ya Burundi unaotarajiwa kuchezwa siku ya Mei Mosi mwaka huu kwenye Uwanja wa Amani mjini Zanzibar.
Timu hiyo yenye jumla ya wachezaji 25 imekuwa ni kivutio kwa Watanzania (Bara na Visiwani) kutokana na uwezo wake ambao imekuwa ikiuoneonesha katika mechi kadhaa ilizocheza na kuwachapa wapinzani wake kwa idadi kubwa ya mabao.
Kabla ya kuichapa Burundi bao 4-0, ‘Serengeti Girls’ ilitoka kuwachapa Botswana kwa idadi kubwa ya magori ikiichabanga mabao 7 kwenye uwanja wa Amani Zanzibar na baadaye kuifuata kwao Botswana ambako ilikung’uta tena mabao 4 -0 na kuzikatisha ndoto za timu hiyo kufuzu kushiriki Kombe la Dunia nchini India mwaka huu.
Ushindi ambao ‘Serengeti Girls’ imekuwa ikiupata unachagizwa na maandalizi mazuri na ushirikiano ilionao kuanzia kwenye benchi la ufundi linaloongozwa na kocha Mkuu wa timu za Taifa za wanawake Bakari Shime, Serikali ya Awamu ya sita na TFF pamoja na wadau wengine wa maendeleo ya mpira wa miguu nchini ambao kwa namna moja ama nyingine wamekuwa ni chachu ya ushindi wa timu hiyo.
Hivi karibuni timu ya Serengeti Girls imekuwa ikizungumzwa na kutizamwa kwa jicho la tatu na mataifa mbalimbali ya Afrika kutokana na kiwango chake kinachoendelea kujionesha katika mashindano yanayoendelea.
Itakubukwa kwamba timu hiyo ya ‘Serengeti Girls’ imewahi pia kutwaa Kombe la COSAFA lililoandaliwa huko Afrika Kusini ambao ilikutana Zambia kwenye mchezo wa fainali (14 Novemba, 2020).
Michuano hiyo ya COSAFA ilianza kutimua vumbi tarehe 4 hadi Novemba 14, 2020.
Timu ya ‘Serengeti Girls’ ya Tanzania ilikwenda kushiriki michuano hiyo kwa mwaliko maalum ikiziwakilisha timu zinazotokea ukanda wa CECAFA ambapo ilifanikiwa pia kutoa mfungaji bora wa mashindano hayo ( Aisha Masaka).