Tff Yaua Ndege Wawili kwa Jiwe Moja
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania TFF kupitia Idara yake ya Ufundi inayoongozwa na Mkurugenzi Oscar Mirambo imewakabidhi vyeti vya kozi ya CAF D Diploma washiriki 51 waliosoma Makao Makuu TFF na wengine 19 kutoka JWTZ Aprili 21,2022.
Zoezi hilo la ufungaji wa kozi sambamba na ugawaji wa vyeti lililofanyika kwenye uwanja wa Uhuru Jijini Dar es salaam liliongozwa na mgeni Rasmi Afisa Mtendaji Mkuu wa Bodi ya Ligi Almasi Jumapili Kasongo akiambatana na viongozi wengine kutoka JWTZ na wengine kutoka TFF.
Akizungumza wakati wa ufungaji wa kozi hiyo CEO Almasi Kasongo amewataka wahitimu hao kujitoa kwa moyo wa dhati kwenda kuyafanyia kazi yale yote waliyopatiwa katika kipindi cha mafunzo yao ikiwa ni sambamba na kujiheshimu kwa wakati wote wa kutimiza majukumu yao kulingana na nafasi waliyonayo katika kukuza mpira wa miguu hapa nchini.
“Moja kati ya mpango kazi wa TFF uliojiwekea ndani ya miaka minne ni kuhakikisha mpira wa miguu nchini unazidi kukuwa kupitia kutoa elimu kwa walimu wengi zaidi ambao watakwenda kuwafikia kwa urahisi vijana ambao watakua ni vizazi vya mpira huo kutoka maeneo tofauti.”
Hata hivyo CEO aliwapongeza wachezaji wa zamani waliowahi kucheza ligi Kuu na wengine waliwahi kutumikia timu ya Taifa ambao pia walikuwa kati ya washiriki kwenye kozi hiyo, sambamba na kuwapatia nafasi 5 za upendeleo washiriki watano kati ya hao 70 ambapo kati yao ni;Athumani Iddi Athumani (Chuji) na Monja Liseki. Pia alisema kuwa Bodi ya ligi itawapatia washiriki wote hao baadhi ya vitendea kazi muhimu kama vile filimbi na vitunza muda kwaajili ya kuanzia wanapokuwa kwenye maeneo yao ya kazi.
Kozi zote hizo zilifanyika kwa siku kumi, kuanzia Aprili 4, 2022 mpaka Aprili 14 mwezi huu huku zikifundishwa na wakufunzi wawili tofauti. Kozi iliyoendeshwa TFF ilifundishwa na Mkurugenzi wa Ufundi TFF Oscar Mirambo na ile ya JWTZ ilifundishwa na mkufunzi RTD Meja A.O.Mingange.